Mbunge wa viti maalum kupitia chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa Rita Kabati ameipongeza Serikali kwa hatua yake ya kuanza kusafirisha Minofu ya Samaki kwenda nje kupitia Mwanza.
Akiongea wakati wa kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Kabati ameishukuru Serikali kwa kuanza kusafirisha minofu ya samaki kupitia uwanja wa ndege wa mwanza na kwamba anaamini kuwa wafanyabiashara wa minofu ya samaki na wadau wote wa sekta ya uvuvi watanufaika.
Aidha amemshukuru Mh. Rais Dkt John Magufuli kupitia Waziri wa mifugo na uvuvi Luhaga Mpina kwa kujenga Machinjio ya kisasa ya Manispaa ya Iringa, kwa kutoa kiasi cha pesa kiasi cha Sh bil.1.1 kwaajili ya kuendeleza mradi huo.
"Toka mwaka 2008 mradi wa machinjio ulikua unasuasua lakini toka nilipomueleza Mh Waziri akachukua hatua kwa kukaaa na watendaji wa Manispaa na kutupatia hizi pesa, kwakweli namshukuru sana".
"Mradi huu ukikamilika utaajiri watu zaidi ya 200 na ajira nyingine ndogo zaidi ya 2000 ikijumuisha wajasiliamali wadogo wakiwemo wasindikaji" Amesema Kabati.
Aidha ameiomba serikali kuvilinda viwanda vya ndani kwa kuongeza ushuru kwenye bidhaa zinazoingia nchini kutoka nje na hasa kwenye bidhaa za Maziwa ili kuongeza tija ya uzalishaji na Ajira kwenye viwanda vya ndani.
"Mh. Naibu Spika, kwa mfano pale Iringa tunacho kiwanda cha kuzalisha Maziwa cha ASAS kiwanda hiki kimekua mfano wa kuigwa na kinazalisha bidhaa bora sana, pia kimeajiiri watu zaidi ya 2000, wakiwemo watu wenye ulemavu, hivyo naiomba serikali iongeze kodi kwa bidhaa za Maziwa kutoka nje ili kuweza kuvilinda viwanda vyetu vya ndani."
Katika hatua nyingine ameiomba Serikali kupitia benki ya Kilimo nchini kuona uwezekano wa kuwasaidia Wavuvi na Wafugaji kwa kupatiwa mikopo kupitia benki hiyo ili Wavuvi na wafugaji waweze kuboresha shughuli zao.
No comments:
Post a Comment