JESHI LA POLISI LABAINI CHANZO CHA AJALI YA BASI LA PRESDAA, LAFUTA LESENI YA DEREVA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Tuesday, June 30, 2020

JESHI LA POLISI LABAINI CHANZO CHA AJALI YA BASI LA PRESDAA, LAFUTA LESENI YA DEREVA



IRINGA.
Jeshi la Polisi Tanzania limebainisha chanzo cha ajali iliyoua watu 10 iliyohusisha kampuni ya Mabasi ya Presdaa inayofanya safari zake kati ya Iringa na Dar es salaam iliyotokea June 27 mwaka huu katika Mlima Kitonga Mkoani Iringa.

Akizungumza na Waandishi wa habari katika eneo la Tukio Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania SAPC Fortunatus Musilim alisema kuwa mara baada ya uchunguzi wamebaini  gari la kampuni hiyo lilikuwa na makosa manne.

Amesema kuwa licha kubaini gari hilo lilikuwa katika mwendo kasi na kuweza kupita kona zaidi ya 37 za mlima kitonga, wamebaini kuwa gari hilo lilikuwa bovu kabla halijaanza safari ya kupeleka abiria kuelekea Jijini Dar es salaam.

Alisema kuwa Kosa lingine walilobaini katika ajali hiyo ni Dereva aliyesababisha ajali hiyo hakuwa mzoefu kutokana na Dereva wa basi hilo kukataa kuendesha basi hilo lililokuwa bovu na kutoa taarifa kwa mmiliki wake.

Aliongeza kuwa kabla ya ajali hiyo Wakala wa Kampuni hiyo alimpigia simu Mmiliki wa Gari hilo na kumwambia kuna abiria wengi katika stend ya mabasi ya igumbilo hivyo kwa tamaa ya kutaka faida bila kufanya ukaguzi wa gari hilo, waliamua kupakilia nje ya stendi hali iliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo.

Aidha SAPC Musilim amemtaka Mmiliki wa gari hilo aliyejulikana kwa jina la Meji Msuya Mkazi wa Dar es salaam kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kufanikisha kumpata dereva aliyesababisha ajali hiyo na yeye mwenyewe kufika katika kituo chochote cha polisi au kufika ofisi za Trafiki makao makuu.

Kamishna Muslim amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya usalama wa barabarani sura ya 168 kifungu cha 36 kidogo cha tano, imesema kuwa ajali inapotokea na kubaini chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa gari, basi mmiliki wa gari atashitakiwa sambamba na Dereva wa Gari.

Ameongeza  kuwa Dereva wa Gari hilo  Said Abas Said anatakiwa kujisalimisha katika kituo chochote cha polisi ili waweze kuchukua maelezo kuhusu ajali hiyo.

Kutokana na ajali hiyo Moja kwa moja  jeshi la Polisi limeisimamisha leseni ya dereva huyo kwa muda wa miezi sita na kuongeza kuwa baada ya dereva huyo kumaliza adhabu yake watampa mtihani wa masuala ya udereva wa kujihami, sheria na usalama barabarani kabla ya kumpa leseni mpya.

Aidha amewataka madereva kafuata sheria za usalama barabarani huku jeshi hilo likiahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wote watakaovunja sheria za na kuongeza kuwa  

wamiliki wa magari ya abiria wanatakiwa kuacha kupeleka magari ambayo ni mabovu ili kuepukana na ajali za barabarani.

Naye Mkuu wa Kikosi cha usalama Barabarani  Mkoa wa Iringa Yusuph Kamota amewataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani hasa wanapokuwa katika katika mkoa wa Iringa kwani kuna milima ambayo ni hatarishi ikiwemo Mlima Kitonga na Mlima Nyang’oro ambayo bila kuwa na uzoefu husababisha ajali.

Kamota aliongeza wamiliki wa Magari waache utaratibu wa kuwapatia madereva wasiokuwa wazoefu wa kutumia barabara hizo na ikiwezekana waombe msaada kwa jeshi hilo hasa wanaokuwa barabarani kujua ni namna gani ya kuweza kupita katika milima hiyo.

Hata hivyo alitoa onyo kali kwa madereva mkoani hapa wasiotaka kufuata sheria za usalama barabarani ni bora wakafanya shughuli nyingine ikiwemo kilimo kwani kwa mkoa huu hawatakuwa salama pindi wakivunja sheria za usalama barabarani.

Katika ajali hiyo ambayo iliyotokea Juni 27 mwaka huu katika Mlima Kitonga imeua watu 10 na kati ya hao Miili ya marehemu watano imechukuliwa na ndugu zao huku majeruhi wa ajali hiyo wakiendelea vizuri na wengine wakiruhusiwa baada ya hali zao za kiafya kuimarika.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages