KATIBU wa NEC, Idara ya Oganaizesheni ya CCM Taifa, Pereira Ame Silima, akitia saini kwenye daftari la watia nia hapo Ofisi KUU ya CCM Zanzibar leo.
KATIBU wa NEC, Idara ya Oganaizesheni ya CCM Taifa, Pereira Ame Silima, Amechukua fomu ya kuwania kugombea Urais wa Zanzibar kupitia Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi ametimiza idadi ya wagombea 27.
Na Mwandishi Wetu Zanzibar.
JOTO la nani atakayepewa kijiti kukiokongoza Zanzibar katika kinyang’anyiro cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) limeendelea kupanda baada ya Kada nguli wa chama hizo Pereira Ame Silima kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Silima licha ya kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Serikali ya Zanzibar ikiwemo Katibu Mkuu wa Wizara za Biashara Masoko na Utalii, Kilimo, Mifugo na Maliasili tangu Machi 2017 hadi sasa amekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dodoma, Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu ndani ya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar Silima amesema kikubwa kilichomsukuma ni nia yake thabiti ya kukuza uchumi wa wananchi wa Zanzibar.
Akifafanua amebainisha kuwa licha ya viongozi waliopo na waliotangulia kufanya kazi nzuri, ameona kuna changamoto katika ukusanyaji mapato ya ndani na kwamba kasi yake haiendani na uwezo wa kuzalisha.
“Nchi inahitaji maendeleo ya kiuchumi yatakayochagiza ukuaji kipato cha taifa na mwananchi mmojammoja, lakini sasa kipato cha wananchi ni kidogo na hivyo wengi kuangukia kwenye umaskini, kama nikipata ridhaa ya kuongoza nitahakikisha taifa linapiga hatua kimaendeleo,” amesema Silima.
Kuhusu kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi, Ame Silima ambaye pia ni Mtaalam wa masuala ya Usimamizi wa Fedha na Biashara za Kimataifa amesema Zanzibar kwa sasa inategemea sekta za Utalii na Bahari kukuza mapato jambo ambalo linahitaji kufanyiwa maboresho.
“Uchumi wa Zanzibar unategemea sekta chache ikiwemo Utalii na uchumi wa bahari ambao haujawekezwa ipasavyo, hivyo kama chama nitachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar jukumu langu la kwanza litakuwa kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya kutosha ya kukuza uchumi,” amesema.
Akizungumzia umoja wa kitaifa amesema kwa sasa Zanzibar inahitaji jamii yenye umoja kuliko iliyopo sasa katika upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu bora, afya na maji, yaani asiwepo wa kumwogopa mwenzake kwa sababu yoyote ile.
“Baadhi ya wanasiasa walitugawa Wanzanzibar kutokana tu na itikadi za kisiasa hadi kufikia watu kuogopana, katika zama zangu kila mtu atakuwa huru kufanya vile atakavyo katika misingi ya kisiasa au kidini ili mradi tu havunji katika ya nchi,” amesema Silima.
Kwa upande wa ustawi wa jamii Ame Silima ambaye ni mtaalam katika Utayarishaji na Uchambuzi wa Sera mbalimbali amesema atatumia uzoefu wake kuhakikisha Zanzibar inakuwa na mkakati maalum wa kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa watoto na wanawake.
Kwa mujibu wa Silima ambaye hadi sasa anafanya idadi ya wanachama waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kufikia 29 ni kuwa, licha ya viongozi waliotangulia kufanya juhudi mbalimbali za udhibiti vitendo hivyo, matokeo hayajawa mazuri kulingana na matarajio ya wananchi.
“Nimechoka kuchagua na kuwa mpiga makofi, sasa naomba ridhaa ya chama na baadae wananchi ili niweze kusimamia hivi vitu mwenyewe, huku nikikuza sekta za kilimo na gesi ambayo haijawa tayari, hata mimi nina mchango mzuri kama nitapata fursa hiyo,” amefafanua Ame Silima.
Pereira Ame Silima aliyezaliwa miaka 61 iliyopita aliyewahi kutunukiwa tuzo ya mwanafunzi bora wa Shahada ya Kwanza ya Misitu kwa miaka mitatu mfululilizo, ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili (MSC) ya Mipango ya Usimamizi wa Misitu (1991) kutoka Chuo Kikuu cha Helsinki, Finland.
No comments:
Post a Comment