Na Salum Humud Salum - Zanzibar
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amesema mashirikiano mazuri yaliopo baina ya Tanzania na China yameleta mafanikio makubwa hasa katika sekta ya Elimu kwa kutoa nafasi mbalimbali za masomo ya Elimu ya juu kwa Wanafunzi wa Zanzibar.
Akizungumza katika hafla ya kuwapokea Wanafunzi wanaotoka nchini China katika ukumbi wa Wizara ya Elimu Mazizini Unguja amesema kupata fursa ya kusoma Elimu ya juu kutasaidia Taifa kuwa na wataalam mbalimbali nchini.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafanya kila jitihada kuhakikisha fursa za Elimu zinazotolewa na Mataifa mengine zinatumika ipasavyo ili nchi iendelee kupiga hatua ya kimaendeleo kwa kuzalisha wataalam wa fani mbalimbali.
Aidha Mhe Riziki amewapongeza Wanafunzi hao kwa kulinda utamaduni wa Zanzibar na kukitangaza zaidi kishwahili kwa kipindi chote cha masomo wakiwa nchini China.
Pia amewapongeza wahitimu hao kwa kuwa wavumilivu katika kipindi kigumu walichopitia cha kupambana na maradhi ya Corona na kuhakikisha wanamaliza masomo yao Salama.
Nae Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe Simai Mohammed Said amewasisitiza wahitimu hao kua wabunifu kwa kile walichojifunza ili waweze kuwasaidia na wengine katika kupambana na suala zima la ajira.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Utawala na Uendeshaji Mwalimu Abdullah Mzee Abdullah amewapongeza Wanafunzi hao kwa kuwa mabalozi wazuri kipindi chote cha masomo na kuifanya Tanzania kutajika vizuri katika Mataifa mengine.
Mkurugenzi Bodi ya Mikopo Zanzibar Bwana Iddi Khamis Haji amesema uzalendo na jitihada ya wanafunzi wanaopata nafasi za masomo nje ya nchi huwasaidia kupata matokeo mazuri kuliko wanafunzi wanaotoka nchi nyengine .
Kwa niaba ya wazazi wa Wanafunzi hao Bwana Mussa Saleh mihambo ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuiwezesha Bodi ya Mikopo kwa kutoa mashirikiano mazuri kwa Wanafunzi katika kipindi chote cha masomo yao na kuomba kuendeleza jitihada hizo ili waweze kuwasaidia na wengine na nchi izidi kupata maendeleo.
Kwa upande wa Wanafunzi waliorejea nchini kutoka masomoni China Nusura Khamis Zuli ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, WEMA na Bodi ya Mikopo Zanzibar kwa kuwa karibu nao zaidi hasa katika wakati mgumu wa maradhi ya Corona.
Jumla ya Wanafunzi 11 wamerejea nchini kutoka masomoni China ngazi ya shahada ya kwanza ya habari na mawasiliano.
No comments:
Post a Comment