Siya Kolisi wa Afrika Kusini kupeperusha bendera ya UN kwa miaka 2 - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Sunday, July 19, 2020

Siya Kolisi wa Afrika Kusini kupeperusha bendera ya UN kwa miaka 2

Siya Kolisi, Nahodha wa timu ya taifa ya raga ya Afrika Kusini ambaye ametauliwa kuwa Bingwa Mchechemuzi kwa ajili ya mpango wa Spotlight.


Umoja wa Mataifa umemtangaza nahodha wa timu ya taifa ya raga nchini Afrika Kusini, Siya Kolisi kuwa mchechemuzi wa dunia wa mpango wa Spotlight unaolenga kujumuisha wanaume katika harakati za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa tangazo hilo leo wakati wa mhadhara wa kila mwaka wa Nelson Mandela ambao hufanyika tarehe 18 mwezi Julai kukumbuka siku ya kuzaliwa kwa rais huyo wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini.

Kolisi anashika wadhifa huo kwa miaka miwili kuanzia tarehe 1 mwezi huu wa Julai mwaka 2020.

Miongoni mwa majukumu yake ni “kuhamasisha umma kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike,” wakati huu ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwanamke 1 kati ya 3 duniani kote amekumbwa na ukatili wa kimwili au kingono.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa katika baadhi ya nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara,  asilimia 76 ya wanawake wamekumbwa na ukatili wakati wa uhai wao na walio hatarini zaidi ni wanawake na watoto wa kike wa pembezoni.

Ukatili mwingine ni watoto wa kike kuozwa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18, huku kila mwaka watoto wa kike milioni 3 katika nchi 29 za Afrika wanaungana na wanawake na wasichana milioni 200 waliokeketwa.

Hali nyingine ya kutisha kabla ya janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, ni mwanamke 1 kuuawa nchini Afrika Kusini kila baada ya saa 3 na kwamba Umoja wa Mataifa unasema kuwa janga la COVID-19 limetumbukiza wanawake na watoto wa kike katika hali mbaya zaidi.

Ni kwa kuzingatia mazingira hayo, Kolisi atakuwa na majukumu ya kupaza sauti kama vile “wanaume, ni jukumu letu kutokomeza ukatili ambao unakumba wanawake na watoto wa kike,” “natoa wito kwa wanaume kukoma kutekeleza ukatili sasa na daima,” “hakuna uhalali wowote wa kufanya ghasia au ukatili wa kingono.”


Ukatili umegusa wapendwa wangu, sasa nina jukwaa la kupazia sauti


Akizungumza baada ya kutambua kuwa anabeba jukumu  hilo la kimataifa wakati huu wanawake na watoto wa kike wanaendelea kukumbwa na ukatili, Kolisi amesema kuwa ni  heshima kubwa na ni jambo kubwa na tofauti mambo aliyozoea kufanya lakini ni jambo linalokuja na wajibu mkubwa.

Amesema kuwa, “lakini naamini kuwa hili ni jambo linalotakiwa kwa mtu mwenye fursa au jukwaa na ni wakati wangu wa kusimama na kutumia sauti yangu kuzungumzia masuala ya kijamii yanayotokea duniani, bila shaka nitafanya kila niwezalo kwa sababu naamini mabadiliko ni muhimu na nina furaha kufanya kazi na mpango wa Spotlight.”

Kolisi amesema kuwa ni wakati wa kutumia jukwaa lake kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia akisema kuwa, “ni jambo ambalo linanigusa, ni kitu ambacho nimeshuhudia kikiwapata wapendwa wangu, na wakati huo sikuwa na sauti, au hata jukwaa la kupazia sauti, lakini sasa ni wakati wa kutumia na kupazia sauti suala hili na kuzungumza moja kwa moja kwa wanaume, na kuanza kuhoji, kuuliza na kujadili hoja hii ambayo huonekana kuwa na ukakasi.”

Sauti zetu zitabadili fikra za wanaume na wavulana


Bingwa huyo mpya wa kimataifa katika kupeperusha bendera ya Umoja wa Mataifa dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto wa kike amesema kuwa, “nadhani ni muhimu sana kwangu mimi mcheza raga kubeba jukumu hili. Sisi huonekana ni wanaume wenye majivuno, tukitunisha misuli yetu na huwa mfano kwa wavulana na watoto wa kiume, kwa hiyo tukipaza sauti na kuwaelewesha umuhimu wa jinsia nyingine ya kike kuwa ni wanawake na wasichana na lazima tuwaheshimu na tuwatendee usawa."

Amesema kwa kufanya hivyo, wanaepusa kurudia makosa ya wazazi wao au vizazi vilivyotangulia. "Na tuwe na mijadala migumu inayopaswa kufanyika, na hivyo watu kufahamu kuwa sisi ni zaidi ya wanamichezo bali tunajali watu ambao wanatulea au wanaotuunga mkono wawe wanaume au wanawake," ametamatisha Kolisi.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages