Naibu waziri Viwanda na biashara Eng.Stella Manyanya akipata maelezo mafupi kutoka kwa Kaimu Meneja TMDA Sonia Mkumbwa Viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma
Kaimu Meneja wa Mamlaka, Kanda ya Kati, akiwa pamoja na maafisa wake wakitoa elimu kwa afisa uhamiaji aliyetembelea banda la TMDA, katika maonesho ya nanenane yanayoendelea katika Jiji la Dodoma, kwa Kanda ya Kati
Afisa elimu kwa umma TMDA kanda ya kati Husein Makame akitoa elimu kwa wateja waliotembelea banda hilo.
SERIKALI imezipongeza mamlaka za dawa na vifaa tiba (TMDA) na kituo cha uwekezaji nchini (TIC) pamoja na mamlaka ya mapato (TRA) kwa namna wanavyotoa huduma bora kwa Watanzania.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma kwenye maonesho ya nanenane na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya alipotembelea mabanda ya Taasisi hizo.
Naibu Waziri Manyanya amesema mamlaka hizo zimekua zikitoa huduma bora kwa wananchi ikiwemo kutoa elimu kupitia vyombo vya habari ambayo imekua njia nyepesi kufikia wananchi kwa haraka.
Akizungumza katika mabanda ya taasisi hizo Mhandisi Manyanya amesema taasisi hizo zimekuwa mstari wa mbele katika kuwafikishia ujumbe wananchi hususan vijijini, hivyo amezitaka kuendelea kuwa na juhudi zaidi katika kuwaelimisha Watanzania .
" Nikiri wazi katika Taasisi ambazo zinafanya kazi nzuri na kuwafikia watanzania basi ni TMDA na TIC niwapongeze sana kwa uelimishaji na utoaji elimu mnaowapatia wananchi wetu hasa wale wa vijijini, endeleeni kuwafikia na kamwe msisubiri maonesho yafike, wafikieni mara kwa mara.
TIC mnafanya vizuri ndio maana hata watanzania wazawa wanachangamkia fursa za kiuwekezaji maana zamani kulikua na kasumba mwekezaji lazima awe mzungu ila nyie mmetoa elimu na mmevutia watanzania kuwekeza kwenye Nchi yao," Amesema Mhandisi Manyanya.
Naibu Waziri pia ameipongeza TRA kwa usimamizi wake wa mapato ambao umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato ambapo sasa Watanzania wamekua wazalendo katika kulipa kodi na yote hiyo imesababishwa na elimu kubwa inayofanywa na mamlaka hiyo.
No comments:
Post a Comment