Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akitoa maelezo mafupi kuhusu maonesho ya nane nane kanda ya Magharibi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuyafunga rasmi.
Mchakataji wa Mazao ya Ziwa Tanganyika kutoka Wilayani Uvinza Raphael Chekwe (kulia) akiwaonyesha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Adengenye(suti nyeusi) na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati( mwenye miwani) samaki aina ya kuku maji aliyechakatwa tayari kwa kusafishwa. Alitoa maelezo hayo wakati viongozi hao walipokuwa wakiembelea mabanda mbalimbali kabla ya maonesho ya nane nane kanda ya Magharibi hayajafungwa rasmi.
WANDAAJI wa maonesho ya nane Kanda ya Magharibi wametakiwa kualika Kampuni na Taasisi za nje ya Kanda hiyo zinazojihusisha na tekonolojia ya zana za kisasa za kilimo, usindikaji wa mazao, ufugaji na uvuvi ili kuongeza wigo wa utoaji wa elimu juu kwa wahusika wa sekta hizo kwa bei nafuu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye wakati akifunga maonesho ya nane nane kwa Kanda ya Magharibi inajumuisha mikoa ya Tabora na Kigoma chini ya kauli mbiu inayosema kwa maendeleo ya kilimo , mifugo na uvuvi , chagua viongozi bora 2020.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuendelea kuboreshwa kwa tekonolojia za kilimo, uvuvi na ufugaji na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi na ajira.
Adengenye alisema Kanda ya Magharibi inazo fursa nyingi za uwepo maeneo makubwa ya uzalishaji wa mazao, mifugo mingi na maeneo ya uvuvi ambayo yakiboreshwa yataongeza myonyoro wa thamani na kuwezesha kupata malighafi bora na za kutosha kwa ajili ya viwanda hapa nchini na nje ya nchi.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Kigoma aliwahimiza wananchi kuongeza juhudi katika ufugaji wa samaki kwa ajili ya kujipatia chakula cha aina ya protini na kujiajiri wenye ili kujipatia kipato chao.
Alisema ni vema wakatumia vema Kituo cha Serikali cha Ukuzaji Viumbemaji kilichopo wilayani Igunga kupata elimu ya ufugaji bora na kununua vifaraga bora vya samaki wa aina mbalimbali kwa ajili ya kufuga.
Katika hatua nyingine Adengenye ameiomba Wizara ya kilimo na ile mifugo na uvuvi kuimarisha mashamba ya mifugo na mimea ili yazalishe mbegu bora za mifugo na mimea kwa ajili ya wakulima na wafugaji.
Aliongeza kuwa ni vema wakasaidia kuimarisha huduma za utafiti , uchunguzi na udhibiti wa magonjwa ya mifugo na mimea ili kuwe na uzalishaji mzuri wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati aliwataka wakazi wa Kanda ya Magharibi kutumia fursa ya uchaguzi Mkuu ujao kuchagua viongozi ambao watakuwa na moyo wa kuwasaidia wakulima , wafugaji na wavuvi kupiga hatua na kushiriki katika uchumi wa kati kikamilifu.
Alisema ni vema wakachagua kiongozi ambaye atakuwa tayari kuwasaidia katika kuwawekea mazingira mazuri ya uzalishaji ili waweze kuongeza vipato vyao.
No comments:
Post a Comment