Rehema Matowo | Mwananchi | Geita | Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita kimepata pigo baada ya madiwani wake wawili wateule kufariki dunia kwa nyakati tofauti wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Bugando jijini Mwanza.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Novemba 7, 2020 katibu mwenezi wa CCM mkoani Geita, David Azaria amewataja madiwani hao wateule kuwa ni Masalu Luponya (Bugalama) na Magomamoto Zanziba (Buziku).
Azaria amesema Luponya aliugua wakati wa kampeni na hata siku ya uchaguzi Oktoba 28, 2020 alipigiwa kura na wananchi akiwa amelazwa hospitali ya Bugando.
Amesema Magomamoto aliugua ghafla juzi na alipelekwa Bugando lakini alifariki saa chache baadaye.
Amesema Luponya atazikwa leo nyumbani kwake Bugalama huku taratibu za mazishi ya Magomamoto zikiendelelea kufanywa na chama hicho kwa kushirikiana na familia yake.
Magomamoto alikuwa diwani wa Buziku kuanzia 2010 hadi 2020 na mwaka 2010 hadi 2015 alikuwa makamu mwenyekiti wa baraza la madiwani.
Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Geita, Jonathan Masele amesema kifo cha Luponya ni pigo kwa CCM na jamii iliyokuwa ikimzunguka.
Luponya wakati wa uhai wake alikua akisomesha wanafunzi 50 wa sekondari na 20 wa ualimu sambamba na kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwenye kata hiyo.
Chanzo: Mwananchi

No comments:
Post a Comment