MBUNGE wa Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo ameamua kuanzisha mpango maalumu wa kuhamasisha somo la hesabu ndani ya jimbo hilo ikiwa ni mkakati wa kuongeza ufaulu.
Katika kuufanikisha mpango huo ambao ameutangaza leo mbele ya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Ummy Mwalimu ,katika kila A ambayo itakuwa inapatikana katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne basi mwalimu wa somo hilo aliyefanikisha mwanafunzi kupata alama A katika hesabu atapewa Sh.100,000.
Akizungumza mbele ya Waziri Ummy Mwalimu, wadau wa elimu na hasa katika somo la hesabu ,madiwani ,walimu, wanafunzi na wazazi ,Profesa Mkumbo amesema matamanio yake ni kuona ufaulu wa somo la hesabu unaongeza katika Jimbo la Ubungo.
Amefafanua katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliopita, wanafunzi hawakufanya vizuri katika somo hilo la hesabu kwani ufaulu uko chini sana,hivyo amekuja na mkakati wa kuhamasisha wanafunzi kupenda hesabu na wakati huo huo kwa walimu ambao watafanikisha wanafunzi kupata alama A watakuwa na motisha mbalimbali.
Amesema mbali ya walimu wa somo la hesabu kupata Sh.100,000 kwa kila A moja ya mwanafunzi, pia watakuwa wanatambua mchango wao kwa kuwatunuku tuzo na vyeti lakini kwa wanafunzi ambao watafaulu kwa kupata alama A ya hesababu na kujiunga kidato cha tano atawalipia ada pamoja na vifaa vingine vinavyohitajika ikiwemo sare ya shule.
Aidha amesema kwa wanafunzi ambao watapata alama B ya hesabu na wakafanikiwa kufaulu kuendelea na masomo ya kidato cha tano atawalipia nusu ada pamoja na kugharamia mahitaji mengine yanayohitajika shuleni.
"Mpango huu ni maalum kwa ajili ya kuinua ufaulu wa somo la hesabu kwa wanafunzi wetu, ufaulu uko chini na hivyo nimeona haja ya kuja na mkakati ambao utatusaidia kuwafanya wanafunzi wetu Jimbo la Ubungo wapende hesabu na wafaulu vizuri.
"Katika mpango huu tutakuwa tukitoa mafunzo ya ndani kwa walimu wetu wa hesabu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , ambapo watalaamu wa somo hilo watakuwa wakiwajengea uwezo walimu wetu na kupeana mbinu za kufundishia hesabu,"amesisitiza Profesa Mkumbo.
Kwa upande wake, Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu amempongeza Profesa Mkumbo kwa kuja na mkakati huo wa kuinua ufaulu wa somo la hesabu wilayani Ilala na kwamba Serikali itatoa ushirikiano hasa kwa kuzingatia tayari imekamilisha mkakati wa kuinua ubora wa elimu nchini kupitia programu ambayo itaanza rasmi Julai 1 mwaka huu nchini kote.
"Kwa hiyo nakupongeza Profesa Mkumbo kwa mpango huu, umetuwahi ,kabla ya sisi Serikali hatujaja na mpango huu.Umeamua kuja na mpango wa kuchochea, kufundisha na kujifunza hesabu, na sisi kama Serikali nini ambacho tunafanya , kuanzia Julai tutaanza kutengeneza programu ya kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari.
"Kwa hiyo tumeanzisha mambo manne ambayo tutayafanya, kwanza kufanya mafunzo kazini kwa walimu wote wa hesabu kuhusu mbinu bora za ufundishaji darasani na jinsi ya kuwasaidia wanafunzi wenye uelewa mdogo, kwa hiyo sisi tutaanza baada ya kupitisha bajeti siku ya Jumatano na Julai tutaanza . Jambo la pili tutachapa na kusambaza vitabu vya hesabu kwa wanafunzi wote wa sekondari ,tunataka kila mwanafunzi awe na kitabu chake ili aweze kufanya mazoezi wakati wote nje ya masomo,"amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Aidha amesema jambo la tatu wanakwenda kulifanya ni kufufua au kuanzisha vituo vya kujifunza vya walimu katika ngazi ya tarafa , na ngazi ya Kata, ili walimu wawe na sehemu ya kwenda kujifunza mada ngumu lakini pia kubadilisha mbinu katika kufundisha hesabu.
"Jambo la nne ni kuhamasisha wanafunzi kupenda hesabu , kwa hiyo nakushukuru Profesa Kitila Mkumbo kwa kuja na mpango huu, lakini umenipa changamoto katika hili la kutoa motisha kwa walimu.Niseme motisha ni muhimu kwa walimu wetu kwani unaweza kuwa na kila kitu lakini kama hakuna motisha inaweza kurudisha nyuma jitihada zote, " amefafanua.
Ameongeza kuwa watoto waliofanya mtihani wa kidato cha nne katika Wilaya ya Ubungo walikuwa zaidi ya 700,000. "Sasa asilimia 10 ya wanafunzi kati ya hao wakipata alama A ya hesabu maana yake mwalimu anakwenda kupata fedha ya kutosha tu atakayoipata kama motisha kutokana na umahiri wake wa kufundisha na kusababisha wanafunzi kupata A."
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo
No comments:
Post a Comment