Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro | Serikali kwa kushirikiana na wadau imepanga kudhibiti Uvuvi haramu kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Mkoani Kilimanjaro.
Haya yamesemwa na Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah leo (28.04.2021) baada ya kumalizika kwa kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu ulinzi na usimamizi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu. Kikao hicho kiliwajumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wilaya za Mwanga, Moshi na Simanjiro kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga.
Dkt. Tamatamah amesema kupitia kikao hicho wamejadili kwa kina kuhusu tatizo la Uvuvi haramu unaofanyika kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na kutoka na maazimio ambayo Wizara na Halmashauri zilizoshiriki pamoja na wadau watakwenda kuyasimamia utekelezaji wake lengo likiwa ni kudhibiti shughuli za uvuvi haramu katika bwawa hilo. Moja ya maazimio hayo ni pamoja na udhibiti wa uuzwaji wa samaki wadogo kwenye masoko yanayosimamiwa na halmashauri.
“Samaki wadogo wanavuliwa pasipo halali na huwa wanauzwa kwenye masoko ambayo yapo chini ya halmashauri, hivyo tumekubaliana wote kuwa baada ya siku saba halmashauri zihakikishe samaki hao hawauzwi tena katika masoko na hii itasaidia kuwafanya wavuvi kupunguza au kuacha kuvua samaki hao kwa kuanza kukosa wanunuzi,” alisema Dkt. Tamatamah.
Dkt. Tamatamah amesema sera ya uvuvi ya mwaka 2015 imekasimu majukumu ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa serikali kuu kwa maana ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya TAMISEMI kupitia Halmashauri na majukumu mengine yamekasimiwa kwa wavuvi na wadau wengine.
Vilevile amesema kuwa Wizara inayojukumu la kutunga sera, sheria na kanuni lakini TAMISEMI kupitia halmashauri zinaowajibu wa kuzisimamia na kuhakikisha kwamba utekelezaji wake unafuatwa. Lakini kwa upande wa wavuvi wanaowajibu wa kushiriki katika ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi kwa kuwa wao ndio wanufaika wa kwanza.
Mkutano huo umewahusisha wadau wa pande zote kwa maana ya wizara, halmashauri na wadau ili kuwa na mkakati wa pamoja badala ya kila mmoja kuwa na mkakati wake kuhusu udhibiti wa uvuvi haramu na kuhakikisha rasilimali za uvuvi kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu zinalindwa na kusimamiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Thomas Apson amesema moja ya changamoto iliyojitokeza katika udhibiti wa uvuvi haramu ni kwamba kila wilaya ilikuwa ikifanya doria kwa wakati wake hivyo wavuvi wakiona doria inafanyika katika wilaya moja wanakimbilia kwenye wilaya nyingine. Lakini kutokana na makubaliano ya kikao, sasa utawekwa utaratibu mzuri wa doria zinazofanyika ili kutotoa tena nafasi kwa wavuvi kufanya uvuvi haramu.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhe. Zephania Chaula amesema moja ya changamoto iliyopo ni ya uingizwaji wa zana haramu za uvuvi kupitia mipakani. Hivyo ameziomba mamlaka zinazohusika kuhakikisha zana hizo hazipitishwi kwani hiyo ni moja ya njia ya kudhibiti uvuvi haramu hapa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulayi amesema kwamba wizara inaendelea kuwahamasisha wavuvi kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kuunganishwa na taasisi za fedha kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambazo zipo tayari kuwakopesha na hivyo wataweza kununua zana sahihi na zenye ubora kwa ajili ya kufanyia shughuli za uvuvi.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akizungumza na wajumbe wa Kikao cha ujirani mwema (hawapo pichani) kilichojadili kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ambacho kimejumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara na Halmashauri za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na Simanjiro. Kikao kimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro. (28.04.2021)
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi (aliyesimama) akifafanua jambo wakati wa Kikao cha ujirani mwema kilichojumuisha Viongozi na Wataalam kutoka Wizara, Halmashauri za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na Simanjiro kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ikiwa ni pamoja na udhibiti wa uvuvi haramu. Kikao kimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro. (28.04.2021)
Baadhi ya Viongozi na Wataalam kutoka Wizara na Halmashauri za Wilaya ya Mwanga, Moshi Vijijini na Simanjiro wakisikiliza mada kwenye Kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu. Kikao kimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kindoroko wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro. (28.04.2021)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga wakati alipofika wilayani hapo kushiriki kikao cha ujirani mwema kilichojadili kuhusu usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Thomas Apson na kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi. (28.04.2021)
No comments:
Post a Comment