Katika muendelezo wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Benki ya CRDB iliandaa futari kwa wateja wake katika mkoa wa Dar es Salaam.
Hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Serena ilihudhuriwa na zaidi ya wateja 400 ikiwamo Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadj Mussa Salum.
Akizungumzia katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo inawachukulia wateja kama sehemu ya familia yake, hivyo Mwezi huu Mtakatifu unatoa fursa ya kushirikiana kuboresha mahusiano kwa kushiriki pamoja katika ibada ya funga na futari.
“Tunatumia kipindi hiki pia kuonyesha shukrani zetu kwao kwa kuendelea kuichagua benki yetu; wakati huo huo tunathibitisha kujitolea kwetu kuelewa mahitaji yao na kuzidi matarajio yao,” alisisitiza Nsekela.
Nsekelea alisema mbali na kufuturisha wateja, Benki ya CRDB pia imekuwa ikitoa msaada wa futari kwa vituo vya kulelea watoto vyenye uhitaji mkubwa. Mwaka huu Benki hiyo imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kusaidia futari kwa vituo vya kulelea watoto 40 katika kanda zote nchini.
Akitoa shukrani kwaniaba ya wageni waalikwa katika hafla hiyo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadj Mussa Salum aliishukuru na kuipongeza Benki ya CRDB kwa kuuandaa futari hiyo, pamoja na kutoa misaada kwa watoto wanaolelewa katika vituo vya watoto yatima katika mwezi huu wa Ramadhan.
“Mafundisho ya Mtume SAW yanatuambia atakayemfuturisha aliye na swaum atapata thawabu kama zake bila ya mwenye swaum kupungukiwa na kitu,” alisema Alhadj Mussa.
Akiwaasa waislamu katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Alhadj Mussa alisema ni vyema walio na uwezo kuwafuturisha wasio na uwezo ili kujiongezea thawabu, lakini pia alisistiza juu ya kusoma Quran kwa wingi, kusali Taraweh na Witri, kukithiri kufanya mema na kujitenga nay ale yaliyoharamishwa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza wakati wa hafla ya futari kwa wateja wake katika mkoa wa Dar es Salaam, iliyofanyika jana kwenye Hoteli ya Serena.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (kulia) akisalimiana na mmoja wa wageni waliohudhuria dhifa hiyo.
No comments:
Post a Comment