KAMATI YA MPITO YA WAZIRI WA AFYA YATOA TAARIFA KUHUSU UCHAGUZI WA BARAZA LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI (NGOs) - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Tuesday, June 22, 2021

KAMATI YA MPITO YA WAZIRI WA AFYA YATOA TAARIFA KUHUSU UCHAGUZI WA BARAZA LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI (NGOs)

Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa viongozi (NaCoNGO) Wakili Flaviana Charles ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea Haki za Binadamu na Biashara, (wa pili kulia) akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wao na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam. (kulia kwake) ni Katibu wa Kamati hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga, (wa kwanza kushoto) ni mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la (WISE) Dkt. Astronaut Bagile, na (wa kwanza kulia) ni Mkurugenzi Shirika la (WiLDAF) Wakili Anna Kulaya.
Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa viongozi (NaCoNGO) Wakili Flaviana Charles (kulia) akijadiliana jambo na Katibu wake Francis Kiwanga (kushoto) wakati wa mkutano wao na waandishi wa Habari uliofanyika Juni 16, 2021.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa NaCoNGO Wakili Fraviana Charles akizungumza na waandishi wa Habari (hawamo Pichani) kwenye mkutano wao na wanahabari hao jijini Dar es Salaam.

DAR ES SALAAM | Kamati ya mpito iliyoteuliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. DK Doroth Gwajima Kusimamia uchaguzi wa Viongozi wapya wa Baraza la Taifa la Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACONGO), imetoa taarifa kuhusu ratiba ya uchaguzi na taratibu muhimu za kuzingatiwa ili kufanikisha uchaguzi huo.

Pia Kamati hiyo imewasisitizia na kutoa rai kwa wadau wa Sekta ya Asasi za Kiraia nchini wakiwemo wanawake na makundi maalum (Watu wanaoishi na VVU, watu wenye Ulemavu) kujitokeza kushiriki kwenye uchaguzi huo ilikupata Baraza jipya la NACONGO ambalo litaundwa na wajumbe kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Flaviana Charles , Mwenyekiti wa Kamati hiyo alitoa muongozo wa ratiba ya uchaguzi, taarifa na kanuni za uchaguzi huo utakaofanyika mwezi Juni 2021 na kumalizika Julai 2021.

"Kamati inapenda kutoa taarifa kwa umma na Mashirika yote yasiyo ya kiserikali ratiba ya uchaguzi na taratibu muhimu za kuzingatiwa ilikufanikisha uchaguzi huo. Fomu zinapatikana kwenye ofisi za Maafisa Maendeleo ya Jamii Wilaya zote nchini kuanzia tarehe 21 Mwezi Juni mwaka huu. Mwisho wa kurudisha fomu za maombi ya nafasi mbalimbali za uongozi ni tarehe 24 Juni.’’ Alisema Flaviana Charles.

Alisema uchaguzi wa Baraza jipya la NACONGO utafanyika katika wilaya zote. Uchaguzi katika ngazi ya Wilaya utafanyika tarehe 26 Juni na Uchaguzi wa wajumbe wa Baraza katika ngazi ya Mkoa utafanyika kwanzia tarehe 28 Juni hadi Tarehe 2 Julai. Uchaguzi wa Mwakilishi wa Mashirika ya Kimataifa; Makundi Maalumu (Watu wanaoishi na VVU, watu wenye Ulemavu, na Watoto) utafanyika tarehe 5 Julai na Uchaguzi wa Viongozi wa Kitaifa wa baraza la NACONGO (Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Mweka Hazina) Pamoja na wenyeviti wa kamati mbalimbali utafanyika tarehe 7 Julai 2021. Hivyo, Baraza jipya la NACONGO litazinduliwa tarehe 9 Julai jijini Dodoma.

Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 inaunda Baraza la Taifa la Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO). Hili ni Baraza huru la Mashirika yote Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yaliyosajiliwa na yanayofanyakazi Tanzania Bara. Baraza linaundwa na wajumbe 30 ambao wanachaguliwa kutoka mikoa yote (26) ya Tanzania Bara pamoja na wawakilishi kutoka makundi maalum.

"NACONGO ni Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini. Ni Baraza muhimu sana kwa uratibu wa kazi zote za NGOs hapa nchini. Baraza hili kwa kawaida linaundwa na wajumbe kutoka mikoa yote 26 na tunatarajia kwa kazi hii ambayo kamati tumepewa tutaifanya kwa makini ili hadi mwezi Julai tarehe 10 tuwe na Baraza hilo jipya’’ Alisema Francis Kiwanga

Ndugu Francis Kiwanga alitoa rai kwa wadau wa sekta ya asasi za kiraia kushiriki kwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ili kupata viongozi wazuri wenye uwakilishi wa mikoa yote katika ngazi za wilaya hadi taifa.

"Sasa rai yetu sisi kama kamati kwa Watanzania na sekta yote ya NGOs nchini ni; tujitokeze kushiriki kwa wingi ili tuweze kupata viongozi wazuri wa Baraza. Ili tufanikishe hili lazima watu wachukue fomu na wagombee kuanzia ngazi ya wilaya, tupate wawakilishi wa mikoa na baadaye tuweze kupata uongozi wa kitaifa."

Pia alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake na makundi maalumu ili baraza jipya liwe na uwakilishi mzuri.

"Ushiriki wa wananwake na makundi maalum ni muhimu sana ndio maana sisi kama kamati tunatoa rai kwa makundi ya wanawake hasa viongozi wanawake waliopo kwenye mashirika ya hapa nchini kujitokeza kutumia fursa hii, ili tuweze kupata Baraza ambalo lina uwakilishi una usawa wa kijinsia na linajumuisha makundi maalum kama inavyosisitizwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu kwamba Asiachwe mtu nyuma. Tunataka Baraza ambalo ni shirikishi zaidi lenye uwakilishi mpana wa wadau wote hapa nchini’’ alisema Ndugu Kiwanga.

Tarehe 7 Juni 2021, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima aliunda Kamati hiyo ya mpito ya watu 10, ambao ni viongozi kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la kusimamia uchaguzi wa viongozi wa Baraza jipya la NaCoNGO kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uchaguzi wa Baraza hilo.

Waziri Dkt. Gwajima alifafanua kuwa kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 38 (1) na (2) cha Sheria ya Mashirika Yasiyoya Kiserikali Na.24 ya mwaka 2002, kuhusu usimamizi wa Sheria hii na utekelezwaji wa kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2016, ameagiza uchaguzi huo ufanyike haraka ili kuwezesha vyombo vya usimamizi wa Mashirika hayo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.

Kwa mamlaka niliyopewa kuhusu usimamizi wa Sheria hii ya utekelezwaji wa Kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali naunda Kamati ya mpito ili kuhakikisha Uchaguzi unafanyika haraka kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi zilizopo." Alisema Dkt. Gwajima.

Kamati hiyo ya watu 10 inaundwa na Flaviana Charles Mwenyekiti wa Shirika Mtandao la Coalition for Women Human Rights Defenders in Tanzania (CWHRDsTZ); Francis Kiwanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS); Dkt. Tulli Tuhuma, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la JSI Research and Training Institute (JSI) ; Edward Porokwa, Mratibu wa Shirika Mtandao la Pastoralist Indigineous Non-Governmental Organizations Forum (PINGOs Forum).

Wengine ni Tike Mwambipile , Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA); Yassin Ally, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini Womens Rights Organization (KIVULINI); Anna Kulaya, Mratibu wa Kitafa wa Shirika la Women in Law and Development Africa (WiLDAF); Audax Rukonge, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agicultural Non State Actors Forum (ANSAF); Gunendu Roy , Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la BRAC Maendeleo Tanzania (BRAC); Dkt. Astronaut Bagile, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Women in Social Enterpreneurship (WISE).

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages