MAJALIWA AWATAKA WANARUANGWA KUZILINDA FEDHA ZA UJENZI WA VETA WILAYA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Monday, June 7, 2021

MAJALIWA AWATAKA WANARUANGWA KUZILINDA FEDHA ZA UJENZI WA VETA WILAYA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoshiriki katika ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Ruangwa kulinda fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa kuvitunza vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameridhia kutolewa kwa fedha za ujenzi huo hivyo ni lazima zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

Ametoa kauli hiyo leo (Juni 7, 2021) wakati alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi.

Rais wetu anatupenda ndiyo maana katuletea pesa ambazo lazima tuzilinde, tukinunua vifaa vya ujenzi kama vile, mabati, saruji, mbao na nondo lazima vyote vitumike hapa kwenye ujenzi na kamwe tusiruhusu udokozi

Waziri Mkuu amesema kuwa serikali itaendelea kuwaletea maendeleo wananchi na yeye akiwa mbunge wao anawajibika kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha Ruangwa inasonga mbele katika nyanja zote.

Pia Waziri Mkuu ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Uongozi wa VETA na Suma JKT kwa kusimamia kwa weledi na uaminifu ujenzi wa chuo hicho na amewataka kuhakikisha kwamba ujenzi unakamilika kwa wakati ili mafunzo yaanze kutolewa.

Akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema chuo hicho kitajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itagharimu shilingi bilioni 2.1 na awamu ya pili itagharimu shilingi bilioni 1.2.

Amesisitiza kuwa mafunzo ya muda mrefu katika chuo hicho yanarajiwa kuanza mwenzi Januari 2022 kwa mujibu wa mafunzo ya VETA.




No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages