Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amethibitisha kuwepo kwa tatizo la wizi wa Mafuta ghafi kupitia Bomba kuu la mafuta Kigamboni na kuamua kuunda Kamati ya siku 10 inayojumuisha Vyombo vya ulinzi na usalama itakayokagua miundombinu hiyo ili kubaini ni wapi wezi wamejiunganishia Mafuta na kusababisha hasara ya Mabilioni ya Shilingi kwa Wafanyabiashara na Serikali.
Akizungumza wakati wa kikao Cha pamoja na Wadau wote wa Mafuta, RC Makalla amemuelekeza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari TPA kununua Vifaa vya Kisasa ya Utambuzi (Radar) vitakavyoonyesha ni wapi Mafuta yanavuja na wezi waliojiunganishia.
Aidha RC Makalla ametoa siku mbili kwa Watu wote Waliojiunganishia Mafuta kujisalimisha kwa Kamati na endapo watakaidi watachukuliwa hatua Kali za kisheria huku akiwataka Wamiliki waliopangisha Nyumba na Viwanja maeneo linapopita bomba la Mafuta kukagua Kama eneo linatumika kwa Wizi.
Pamoja na hayo RC Makalla amesema taarifa zinaonyesha kwa Mwaka kumekuwa na upotevu wa Lita milioni 22 na kumpelekea hasara ya Shilingi bilioni 37 kwa Mwaka, Bilioni 3 kwa Mwezi na Milioni 100 kila siku Jambo linalosababisha hasara kwa Wafanyabiashara na Serikali kukosa Mapato.
Hata hivyo RC Makalla amesema licha ya Wizi huo kusababisha hasara kiuchumi kwa Wafanyabiashara na Serikali, pia inahatarisha usalama maana Bomba wanalotoboa ikitokea mlipuko unaweza kusababisha majanga makubwa kwa Wananchi.
Kikao hicho kimehusisha Watendaji kutoka Taasisi Mbalimbali ikiwemo TPA, TRA, WMA, Wakala wa uagizaji Mafuta kwa pamoja, Wamiliki wa vituo vya Mafuta, umoja wa Wauzaji Mafuta na Wadau wengine ambapo kikao hicho kimekuwa na mafanikio makubwa.
No comments:
Post a Comment