Na Ibahim Mkondo | Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Sheikh Ponda Issa Ponda amefurahishwa na ziara ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu, katika gereza Kuu Ukonga jijini Dar es Salaam na kukutana na Masheikh wanaotuhumiwa kwa Ugaidi.
Sheikh Ponda alifahamu ziara ya Mkurugenzi huyo baada ya kufanya ziara katika gereza hilo na kukutana na watuhumiwa hao.
Sheikh Ponda anasema Mahabusu hao wamemueleza kufurahishwa kwao na ziara ya Mkurugenzi huyo aliyoifanya gerezani kwao mwishoni mwa wiki iliyopita.
Masheikh hao (hasa wale wenye kesi ambazo hazijaanza kusikilizwa), wamesema kuwa ziara hiyo imefufua matumaini yao ya kuanza kusikilizwa kesi zao ambazo kwa zaidi ya miaka minane (8), hazijaanza kusikilizwa kwa madai ya kutokamilika upelelezi.
Walimueleza Sheikh Ponda kuwa DPP, alifika gerezani hapo siku ya Jumamosi ya tarehe 12.06.2021, majira ya saa nne asubuhi na kufanya maongezi nao yaliyodumu kwa takriban masaa mawili na nusu.
Walimuambia kuwa katika jumla ya yaliyojiri kwenye kikao hicho ni pamoja na DPP, kupokea risala ya changamoto zao na wenzao walioko mikoani. Mahabusu hao wamesema baadhi ya hoja zao alizitolea majibu na baadhi aliahidi kuzifanyia kazi kwa haraka.
Aidha Sheikh Ponda amemtaka Mkurugenzi huyo kuonesha tofauti yake na mtangulizi wake kwa kurekebisha mambo kadhaa yanayo wanyima wananchi haki za msingi. Miongoni mwa hayo ni kuwakamata watu na kuwafikisha Mahakamani kabla yakukamilisha uchunguzi na kupata ushahidi. Amesema madai ya kutokuwa na ushahidi hayakidhi hoja za kisheria, mantiki wala haki.
Akitoa mfano Sheikh Ponda amesema mtu aliye muuwa mtu hadharani hukaa gerezani miaka mingi kwa madai ya kutafuta ushahidi. Amesema uchunguzi wa daktari katika tukio la mauwaji ya namna hiyo ndio ushahidi mkubwa na uchunguzi huo hukamilika ndani ya muda wa saa moja au zaidi kidogo.
Amesema mtuhumiwa wa mauwaji ya namna hiyo hukaa gerezani kwa miaka mingi ingawa amekiri kutenda mauwaji hayo mbele ya mpelelezi na maiti amekwishazikwa kwakuwa ushahidi wa daktari umekamilika.
Sheikh Ponda amemtaka Mkurugenzi huyo mpya kuhakikisha kesi za ugaidi zilizowajaza Waislamu magerezani katika mikoa mingi zinaanza kusikilizwa. Amesema sera ya kukaa na mashauri bila ya kuzungumzwa na kuwarundika watu magerezani kwa hoja ya kutafuta ushahi aiondoe ofisini kwake ili kumsaidia Raisi wake kulipeleta taifa katika utawala wa haki na ubinadamu.
No comments:
Post a Comment