
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika majadiliano na Watendaji wa Taasisi mbali mbali za Serikali Ofisini kwake Vuga, Zanzibar.
Watendaji wa Taasisi mbali mbali za Serikali wametakiwa kuwajibika ipasavyo ili kumaliza mrundikano wa Kesi za Udhalilishaji Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa agizo hilo katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji mbali mbali za Serikali zinazoshughulikia masuala ya udhalilishaji kilichofanyika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Taasisi zinazosimamia Kesi hizo zina watendaji wenye ujuzi na uzoefu ambapo uwajibikaji wao utasaidia kutokomeza Janga hilo Nchini.
Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa Jamii ya wazanzibari ina Imani na Serikali yao ambapo kufikia mwisho kwa Kesi hizo kutasaidia Zanzibar kuwa Salama na yenye maendeleo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuwataka watendaji hao kutotumia kesi hizo kwa kumuonea mtu au kumpendelea yoyote bali watende haki kwa kusimamia Viapo walivyoapa kumsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Kwa upande wake Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Awadh Juma Haji ameeleza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea na kuwasaka wahusika wa vitendo vya udhalilishaji pamoja na mashahidi ambao wanakataa kufika mahakamani kutoa Ushahidi kwa makusudi au kwa muhali.
Nae Naibu Mrajis wa Mahkama kuu Zanzibar Salum Hassan Bakari ameeleza kuwa Mahkama imeweka Mikakati madhubuti ya kuungana na Rais Dkt Mwinyi kuhakikisha Janga la udhalilishaji linamaliza Nchini akitolea Mfano mashauri kusikilizwa kwa wakati pamoja kupitia Majalada kuona kesi zilizochukua muda mrefu ziweze kumalizwa.
No comments:
Post a Comment