UONGOZI wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) umekutana na wadau mbali mbali wa utalii kujadili umuhimu wa bima kwa watalii wanaoingia visiwani Zanzibar.
Katika mkutano huo ulioongozwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, ZIC imepokea michango mbali mbali juu ya namna bora ya kuiimarisha huduma hiyo mpya inayotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Septemba 2024.
Wakati akifungua mkutano huo uliofanyika mapema leo katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip Airport Waziri Dkt. Saada Mkuya alisema kuwa Serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa kugharamia matibabu kwa watalii ambao hupata matatizo ya kiafya, gharama ambazo zingeweza kuepukika kwa kuwepo kwa bima ambayo itafidia matatizo hayo pale yanapotokea kwa watalii.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZIC, Bw. Jape Ussi Khamis amesema ni jukumu la kila mdau kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa huduma hiyo ili kufikia malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuvifanya visiwa vya Zanzibar kuwa sehemu salama kwa watalii hata pale majanga yasiyotarajiwa yanapotokea.
Huduma hii mpya itakwenda kuwapatia watalii msaada wa dharura endapo watapata majeraha wakati wakitembelea vivutio vyetu, itawawezesha kupata msaada wa haraka endapo watapoteza hati za kusafiria pamoja na kugharamia kurudisha mwili wa mtalii endapo atafariki ndani ya visiwa vya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment