Dkt.Dimwa - Akemea Rushwa Mchakato wa Kura za Maoni - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Monday, April 14, 2025

demo-image

Dkt.Dimwa - Akemea Rushwa Mchakato wa Kura za Maoni

IMG-20250412-WA0245
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohaned Said Dimwa,akizungumza na Wajumbe wa Kamati za siasa za CCM ngazi za matawi, wadi, majimbo na Wilaya ya Kati pamoja na Kusini Unguja katika ziara ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC, CCM Taifa Zanzibar ya kuimarisha Chama Cha Mapinduzi katika Wilaya hizo kichama.

Na.Is-haka Omar - Zanzibar.

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar,kimesema hakitovumilia vitendo vya rushwa na ubabaishaji katika mchakato wa kura za maoni za uteuzi wa wagombea wake wataotarajiwa kugombea katika uchaguzi mkuu wa dola octoba, mwaka 2025.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, katika ziara ya Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC, CCM Taifa Zanzibar akizungumza na Wajumbe wa Kamati za siasa za matawi, wadi, Jimbo na Wilaya za Kusini Unguja kichama.

Dkt.Dimwa, amesema CCM itachukua hatua kali za kimaadili na kinidhamu kwa wanachama, viongozi na watendaji watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kupokea au kutoa rushwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama.

Alisema kila mwanachama atapata haki ya kuteuliwa kuwa kiongozi katika nafasi zinazowaniwa kwa njia ya haki, usawa, vigezo na taratibu zilizowekwa Chama Cha Mapinduzi na sio makundi ya watu wachache kwa maslahi binafsi.

Katika maelezo yakeDkt.Dimwa, ameeleza kuwa CCM tayari imetangaza rasmi mchakato wa ndani ya chama wa kura za maoni wa kuwania nafasi za kugombea ubunge, uwakilishi na udiwani katika uchaguzi wa dola octoba mwaka huu, ambao fumu zitaanza kutolewa kuanzia Mei 1 hadi Mei 15 mwaka 2025.

Aliwasihi wanachama wote wenye nia ya kuwania nafasi hiyo wajitokeze kwenda kuchukua fomu kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa ili kuimarisha demokrasia ndani ya Chama.

Alisema, hiyo ni fursa kwa wanachama wa makundi yote kushiriki katika mchakato huo ili waweze kupata nafasi za uongozi kwa njia halali na zenye ushindani kwa dhamira ya kuwatumikia wananchi.

"Kila mwanachama ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika mchakato ya ndani ya Chama, utaratibu huu unaruhusu ushindani na hatimaye vikao vya juu vinafanya maamuzi ya mwisho ya uteuzi kwa mujibu wa sifa za kila mgombea" alisisitiza Dkt.Dimwa.

Kupitia ziara hiyo alifafanua mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 yaliyofanyika katika Mkutano mkuu maalum wa januari 18 hadi 19, mwaka 2025 ya kuongeza idadi ya wapiga kura kwenye vikao vya kura za maoni kwa wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani.

"Mabadiliko haya ya kikatiba yanalenga kuongeza uwazi na ushitikishwaji wa wanachama wengi zaidi katika mchakato wa uteuzi wa wagombea, hatua itakayopunguza malalamiko ya upendeleo katika kuwapata viongozi bora wa kuongoza wananchi" alifafanua Dkt.Dimwa.

Aidha,amekemea tabia ya baadhi ya makatibu wa matawi ya CCM kuacha tabia ya kubadilisha mabalozi kwa kipindi hiki, kwani mabalozi wote wa CCM wapo katika mfumo rasmi wa Chama na wamepewa vitambulisho.

Pia ametoa onyo kali kwa baadhi ya wanachama wa CCM wenye nia ya kuomba ridhaa ya uongozi,kuacha tabia ya kuwatisha,kuwakatisha tamaa na kuwazushia uongo viongozi wa ngazi za juu kuwa wamewatuma kugombea.

"Kupitia ziara hii nasema rasmi kuwa kuna baadhi ya wanachama wameanza kudai eti wametumwa na Rais,Katibu Mkuu wa CCM,Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar na wengine ili wagombee,naomba mjue sisi hatujamtuma mtu wasitumie uongo na yeyote atakayebainika Kamati za maadili zitashughulika naye." alisema Dkt.Dimwa.

Naye Katibu wa Kamati maalum ya NEC, idara ya organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi, amewataka wanachama na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa dola octoba 2025, ili CCM ipate ushindi mkubwa na kuendelea kuongoza nchi kwa mafanikio.

Kilupi,alisema matarajio ya CCM ni kupata ushindi wa zaidi ya 90 kutokana na idadi kubwa ya wanachama wake waliojitokeza kwa awamu zote za uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura nchini.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages

Contact Form

Name

Email *

Message *