Kila mwaka
ifikapo Machi 8 kila mwaka, wanawake duniani kote huadhimisha siku yao ambapo
hujitathmini kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo walizofanya, changamoto
zilizopo na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo.
Akiongea
hivi karibuni katika kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, Katibu
mkuu wa Wizara ya Afya na Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi
Sihaba Nkinga alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya
Viwanda; Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko”
Kauli mbiu
hii inasisitiza kuwajengea wanawake uwezo wa kitaaluma, kibiashara, upatikanaji
wa mitaji, masoko na biashara ili waweze kushiriki kwa usawa, na kunufaika na
fursa zilizopo badala ya kuwa wasindikizaji.
“Ujumbe wa
kauli mbiu hii umezingatia sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka
2000 na ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu hususani lengo namba 5 kuhusu
usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi” alisema Bi Nkinga.
Kauli mbiu
ya mwaka huu imetotolewa kutokana na kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa (UN)
isemayo “Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.
Akizungumza
hivi karibuni, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) Mama
Edda Sanga alisema kuwa wanawake wanapaswa kujiwezesha katika maeneo ya
kiuchumi, kisiasa, na kijamii ili wapate fursa ya kushiriki katika maamuzi
mbalimbali ambayo hatimaye yatawaletea tija na mafanikio.
Hii ina
maana kuwa, endapo wanawake watapata nafasi ya kushiriki katika maamuzi
mbalimbali ni rahisi kwao kusikilizwa na hata kuwa na sauti katika masuala ya
wao kumiliki ardhi, majumba na hata viwanda.
Aidha,
kauli mbiu hii inawahamasisha wanawake kuhakikisha kuwa kunakuwa na usawa wa
jinsia unaoondoa vikwazo na kuhakikisha wanapata fursa sawa na kuweka
ulinganifu katika ushiriki ambao unawanufaisha kiuchumi kuanzia ngazi ya
familia.
Ili kufikia
malengo ya kujikomboa kiuchumi, wanawake wanatakiwa kujitambua na pia kutambua
malengo na mipango yao.
Wanatakiwa
kutambua na kutumia fursa vizuri wanayopata hasa mahali watakapopata taarifa za
kuwanufaisha kiuchumi kwa mfano benki, vikundi vya mikopo, taasisi au hata kwa
watu binafsi.
Kumekuwa na
juhudi mbalimbali za kuwakwamua wanawake kiuchumi, kutoka kwenye taasisi,
mashirika na watu binafsi, hata hivyo wao pia wanahitaji kujikomboa kwa
kutumia juhudi zao binafsi kama vile kujiunga katika vikundi waweze kukopeshwa
ili waweze kujiajiri katika mkondo wa uzalishaji mali, kama vile kuanzisha
viwanda vidogo vidogo, kwa mfano viwanda vya usindikaji vyakula, kazi za mikono
na ushonaji ambavyo havihitaji mtaji mkubwa.
Hii
itawafanya kunufaika na kuondoa hali ya utegemezi katika jamii, na hivyo
kujiondoa katika hali ya unyonge.
Ni ndhahiri
wanawake ndio wazalishaji wakubwa katika nyanja za kiuchumi, hivyo katika
kutimiza ndoto na malengo zao ni budi juhudi zitumike ili washiriki katika
kukuza pato lao na taifa kwa ujumla.
Naye Bibi
Lilian Liundi ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) anasema
kuwa katika kusherekea siku ya wanawake duniani, taasisi yao ilifanya
kongamano hivi karibuni pamoja na mambo mengine walizungumzia
mpango wa taifa kuhusu ushiriki wa wanawake katika kuelekea uchumi wa viwanda
vya kati.
Alisema
kuwa wanawake wa mjini kwa sasa wanashiriki vizuri katika shughuli ambazo huwaongezea
kipato wakati wanawake wa vijijini ushiriki wao katika shughuli za kuwaongezea
kipato si wa kuridhisha kwani wanatumia muda mrefu kutembea kutafuta maji na
kuni kwa ajili ya matumizi ya familia.
Bibi Liundi
alitoa wito kuwa huduma za jamii zisogezwe karibu na jamii ili wanawake ambao
ni wazalishaji mali wakubwa wapate muda wa kutosha kushiriki katika shughuli za
kujiongezea kipato badala ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Naye Bibi
Magreth Dotto ambaye ni Mhandisi wa Migodi, na Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo
Kikuu cha Dar-es-salaam aliwashauri watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi kwa
kuzingatia kasi ya ukuaji wa teknolojia kila siku ili baadaye wapate nafasi
nzuri katika jamii na kutoa mchango wao katika kutatua changamoto za kijamii na
taifa.
“Uhandisi
unawezekana kwa wasichana na ni taaluma nzuri, hivyo wasichana waache kuyaogopa
masomo ya sayansi, ni taaluma inayobadilisha maisha kwa kuyaboresha kwa sababu
inalipa vizuri” alisema Bibi Magreth.
Kwa upande
wake Dkt. Ave Maria Samakafu ambaye ni Mhadhiri katika Chuo cha Sayansi ya Tiba
Muhimbili na Mratibu wa Taifa wa Taasisi ya Wanawake ya Ulingo alisema kwa sasa
wanawake wana mwamko mkubwa ambao umeleta mageuzi katika familia na kuinua
kipato chao.
“Kwa sasa
tunaona ushiriki mkubwa wa wanawake katika nyanja ya uchumi kwa sababu kuna
wanawake wafanyabiashara wadogowadogo, wa kati na hata wakubwa” anasema Dkt
Semakafu.
Alisema
kuwa elimu inahitajika zaidi kwa wanawake wa vijijini ambao bado wanatawaliwa
na tafsiri potofu ambapo ukandamizaji wa wanawake bado unapewa nafasi kubwa na
jamii, hivyo kuwafanya wasisonge mbele katika kujiletea maendeleo yao.
Dkt.
Semakafu aliendelea kusema kuwa wanawake wengi wa mjini wanatambua nafasi zao
katika jamii, hivyo wanatumia ufahamu huo kama fursa kwao ambazo zinawasaidia
katika kuleta mageuzi ndani ya familia zao.
“Vijana wa
kike wamekuja na nguvu mpya, kinachoendelea sasa hivi kinafungua uelewa wa
jamii, watoto na wazazi na kuwafanya watambuliwe na jamii” alisema Dkt.
Semakafu.
Dkt.
Semakafu alitoa mfano unaodhihirisha nafasi ya mwanamke akimtaja Agnes Magongo
ambaye hivi karibuni ameshinda tuzo ya UN ya “women economic empowerment”
ambayo ni tuzo ya uwezeshaji wa wanawake.
“Wanawake
tushiriki katika kuboresha maisha yetu, tusiwe wasindikizaji bali watendaji,
twende pamoja katika uchumi wa viwanda ili tuweze kumiliki viwanda” alimalizia
Dkt. Semakafu.
Katika
kuhimiza fursa za uchumi kwa wanawake kauli mbiu ya mwaka huu inalenga
kuhamasisha jamii na wadau wote nchini kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake
ili waweze kushiriki na kunufaika nazo hasa kipindi hiki ambapo Tanzania
inaelekea azma ya uchumi wa kati kwa misingi ya kuwa nchi ya viwanda.
Mama Sihaba
aliwakumbusha wadau wote katika ngazi zote kuweka mikakati thabiti ya kutatua
changamoto zinazokwamisha kufikiwa kwa usawa wa jinsia na kusababisha wanawake
na wasichana kushindwa kutimiza malengo na ndoto zao kimaisha.
No comments:
Post a Comment