Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
Kuanzia 02 Machi, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alianza ziara ya kikazi ya siku 4 katika
Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara iliyolenga kutembelea miradi mbalimbali ya
maendeleo na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Ziara hiyo kwa kiasi kikubwa imeonesha dira na
mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano hasa katika utekelezaji wa miradi
inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali Imani,kabila na itikadi za
vyama vyao vya siasa.
Siku ya kwanza ya ziara yake Rais Dkt. Magufuli
aliweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Tanzania
Goodwill Ceramic Tiles Ltd. kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani ambacho ni kikubwa
Afrika Mashariki na Kati kilichogharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu
ya kwanza.
Akiongea katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi
katika kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku
Rais Magufuli alifurahishwa na teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea
vigae inayotumiwa na kiwanda hicho na kuhoji kama kuna haja ya serikali
kuendelea kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi.
Rais Magufuli alisema kuwa “Nchi hii tumechezewa
vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto
1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake
hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku
kusafirisha mchanga nje ya nchi".
Akiwa njiani kuelekea Mikoa ya Lindi na Mtwara Rais
Magufuli alizungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo
amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa
na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5, unaanza
kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi wa tatu na kupiga marufuku utozaji wa
ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa mazao.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli anawataka wananchi
kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha katika
kipindi hiki mvua zinaponyesha huku akiweka bayana kuwa Serikali haitatoa
chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula
katika maeneo yao.
Akioneshwa kutoridhishwa na utekeleaji wa miradi
inayogusa maisha ya wananchi alipotembelea ujenzi wa mradi wa maji wa Ng'apa
Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika tangu tarehe 17 Machi, 2015 Rais
Magufuli aliagiza kushikiliwa kwa hati za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya
ukandarasi ya Overseas Infranstructure Alliance Private Limited ya India Bw.
Rajendra Kumar pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo
itakapokamilisha mradi huo unaotarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo
milioni 5 za maji kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa
na tatizo kubwa la maji.
Katika kuthibitisha amedhamiria kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya viwanda Rais Dkt. Magufuli aliitaka Wizara ya Nishati na Madini
Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha inafikisha gesi katika kiwanda hicho
haraka iwezekanavyo lengo likiwa kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na
ukosefu wa gesi ambavyo vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama
mara kwa mara.
Aidha, Dkt. Magufuli aliitaka Wizara hiyo
kuhakikisha wanamega eneo lenye makaa ya mawe katika eneo la Ngaka lililopo
Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni ya Dangote ili iweze
kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda chake cha saruji kilichopo
Mkoani Mtwara.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Alhaji Aliko
Dangote tangu kianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo sokoni imeshuka kutoka
Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi kufikia Shilingi 10,000/- na
ununuzi wa magari 580 yatasaidia kusafirisha saruji nchi nzima kwa gharama
nafuu ambayo watanzania wengi wataimudu.
Wakati akikamilisha Ziara yake Mhe. Dkt. Rais
Magufuli alifanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mjini Mtwara
ambapo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inasukuma
maendeleo ya Nchi kwa nguvu kubwa kwa manufaa ya wananchi.
Rais Magufuli alisema kuwa Serikali ya awamu ya
tano imedhamiria kutilia mkazo juhudi za uendelezaji wa bandari ya Mtwara,
ujenzi wa barabara, uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya umeme, ujenzi wa
viwanda vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kilimo ambavyo vitasaidia
kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli alioneshwa kusikitishwa
na Mkoa wa Mtwara kufanya vibaya kielimu na kuwataka kuweka msisitizo katika
elimu kwani juhudi za Serikali kuwapelekea maendeleo hazitakuwa na maana kama
wananchi watakuwa hawana elimu.
Ziara hiyo ya Rais
Dkt. Magufuli imeonesha mwelekeo wa Tanzania tunayoitaka hasa katika maeneo ya
usimamizi wa miradi na utekelezaji wake kwa maslahi ya umma.
No comments:
Post a Comment