Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara,
imemhukumu muuguzi Irene Machagge, kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa
faini ya sh 600,000 baada ya kumtia hatiani kwa kughushi cheti cha elimu ya
sekondari na kukitumia katika ajira.
Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa vyombo vya habari ilisema khukumu hiyo
ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Karim Mushi baada ya kusikiliza
ushahidi wa mashahidi wane wa upande wa mashataka
na mshtakiwa.
Akitoa adhabu hiyo, Hakimu Mushi
alisema amezingatia utetezi wa mshtakiwa, hivyo kumhukumu kulipa faini ya sh
500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kwanza, na la
pili kulipa faini ya sh 100,000 au kwenda jela miaka mitatu.
Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani kwa
mara ya kwanza Novemba 15, 2015 akikabiliwa na mashataka mawili ya kughushi
cheti cha elimu ya sekondari na kukitumia kujipatia ajira ya uuguzi katika
Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Ilidaiwa mahakamani na upande wa
mashtaka kuwa kati ya Mei na Septemba, 2009 alighushi cheti cha kuhitimu Shule
ya Sekondari ya Forodhani mwaka 1995. Na septemba 3, 2009 aliwasilisha cheti hicho
kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara na kuajiriwa kama muuguzi katika hospitali ya
Mkoa.
Hata hivyo, mshtakiwa aliiomba Mahakama
imuonee huruma kwa kuwa ana ujauzito na ana ugonjwa ambao haumruhusu kukaa
kwenye eneo lenye joto kali, hivyo alilipa faini ya sh 600,000 na kukwepa
kwenda jela.
No comments:
Post a Comment