Waziri
Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam
Desalegn (katikati) akifurahia zawadi ya picha ya Bandari ya Dar es Salaam mara
baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Prof. Ignas
Rubaratuka (kulia). Kushoto ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Kassim Majaliwa.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA mara baada ya kuwasili bandari ya Dar es
Salaam kumpokea mgeni wake Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn hivi karibuni.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA mara baada ya kuwasili bandari ya Dar es
Salaam kumpokea mgeni wake Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Desalegn hivi karibuni.
Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mhe.
Hailemariam Desalegn amesema Shirika la Meli la Ethiopia (Ethiopian Shipping
Line) lipo tayari kuanza kuitumia Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kutoa
huduma nzuri.
“Shirika letu la Meli ambalo ni la kihistoria na lililobaki pekee
katika ukanda wa Afrika likiwa linamilikiwa na Serikali ya Ethiopia sasa lipo
tayari kufanyakazi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania,”amebainisha
Mhe. Desalegn.
Ameongeza kuwa mbali na shirika hilo la meli kuwa tayari kuanza kuleta
meli zake Bandari ya Dar es Salaam pia Shirika Kongwe la Ndege la Ethiopia
(Ethiopian Airline) lenye mafanikio makubwa nalo litaanza kusafirisha mizigo
inayopitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine Mhe.Desalegn amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa
na Menejimenti ya TPA katika kuboresha huduma zake ambapo amesema jitihada hizo
sio tu zitanufaisha Serikali zote mbili bali pia ustawi wa maisha ya watu wa
Tanzania na Ethiopia nao utaimarika.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
amemshukuru Waziri Mkuu wa Ethiopia kwa kuja nchini ambapo amemuahidi kwamba
mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili yatadumishwa kwa maslahi
mapana ya mataifa yote.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu wa Tanzania,Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema TPA itaendelea na mipango
iliyopo ya kuhakikisha inaboresha Bandari zake ili ziweze kuhudumia vyema
wateja wote kwa wakati.
“Tutaendelea kuboresha huduma zetu za Bandari na za sekta ya uchukuzi
kwa ujumla ilituweze kufikia malengo yenu na wateja wetu ya kuhakikisha kwamba
tunawahudumia vizuri na kwa ufanisi,” amesema Mhe. Mbarawa.
Mapema akitoa taarifa ya utendaji wa Mamlaka, Mkurugenzi Mkuu wa TPA,
Mhandisi Deusdedit Kakoko alimweleza Waziri Mkuu wa Ethiopia kwamba kwa sasa
TPA inaendelea na mpango wake wakujenga uwezo wa kuhudumia wateja wake kwa
kuzingatia kwamba sekta ya uchukuzi inakuwa kwa kasi.
“Kutokana na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi nchini na Duniani kwa
ujumla, TPA inaimarisha uwezo wake wa kuhudumia mizigo na meli kubwa ilikujenga
uwezo kabla ya mahitaji makubwa kujitokeza”, amesisitiza Mhandisi Kakoko.
No comments:
Post a Comment