Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakiweka saini Nyaraka yenye maelezo ya
masuala yote yaliyokubaliwa katika kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda.
Waziri Mahiga na
Mgeni wake, Mhe. Sam Kutesa wakionesha nakala za nyaraka za makubaliano mara
baada ya kusaini.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakiweka saini Mkataba utakaotoa fursa kwa Tanzania na
Uganda kushirikiana katika huduma za usafiri wa anga.
Prof. Mbarawa na Mhe.
Kutesa wakionesha nakala za mikataba mara baada ya kuisaini.
Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa
Nishati na Madini wa Uganda, Mhe. Mhandisi Irene Muloni wakiweka saini Mkataba
ambapo Tanzania na Uganda zitashirikiana kuendeleza mradi wa umeme wa kutumia
maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo.
Waziri Mahiga na
Mhandisi Muloni wakibadilishana nakala za mikataba.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Ramadhan Mwinyi ambaye alikuwa mwongozaji wa kikao cha Tume ya Kudumu ya
Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kwa ngazi ya Mawaziri kati ya Tanzania na Uganda
akitoa neno la ukaribisho kwa wajumbe waliohudhuria kikao hicho.
Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisoma
hotuba ya kufunga kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda.
Waziri wa Mambo ya Nje
wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa akisoma hotuba kwa wajumbe walioshiriki kikao cha
JPC kati ya Tanzania na Uganda.
Baadhi ya Viongozi
waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioshiriki kikao
cha JPC kati ya Tanzania na Uganda. Wa kwanza kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi na wa pili ni Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
Ujumbe wa Tanzania
ukifuatilia hotuba za Waheshimiwa Mawaziri wa Mambo ya Nje
Viongozi wa ngazi ya
juu wa Serikali ya Uganda wakisikiliza hotuba za Mawaziri.
Ujumbe wa Tanzania
ukifuatilia mkutano
Bw. Gerald Mbwafu
(kulia) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa
Masuala ya Maji, Bw. Sylvester Matemu kutoka Wizara ya Maaji.
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo
ya Nje wakionesha nyuso za furaha kuashiria furaha yao baada ya kufanikisha
mkutano wa JPC.
Tanzania na Uganda zimefungua sura mpya ya ushirikiano baada ya
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo kusaini nyaraka inayoainisha maeneo
mbalimbali ambayo nchi hizo zimekubali kushirikiana kwa pamoja ili kuinua
uchumi wa mataifa yao.
Nyaraka hiyo iliyosainiwa leo jijini Arusha imetokana na Kikao cha Tume
ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda
kilichofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 03 Aprili 2017.
"Makubaliano haya yataongeza chachu ya uhusiano na ushirikiano
wetu na Uganda, japokuwa tulichelewa kufanya kikao cha JPC tokea mkataba
uliposainiwa mwaka 2007 nchini Uganda". Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga alisema alipokuwa
akisoma hotuba ya kufunga.
Kikao cha JPC kilifanyika kwa kuzingatia makundi ya kisekta ambapo
katika kila kundi, wajumbe waliainisha maeneo yenye maslahi kwa pande zote
ambayo yanajumuisha pamoja na mambo mengine: uendelezaji wa miundombinu;
kilimo; viwanda; biashara; uwekezaji; nishati; utalii; utunzaji wa mazingira;
uvuvi; ufugaji; afya; elimu; utangazaji; madini na masuala ya kijamii.
Kikao hicho kilitarajiwa kuhitimishwa kwa kusainiwa mikataba sita
lakini kutokana na mashauriano ya ndani ya baadhi ya mikataba kutokamilika,
mikataba miwili ndio iliweza kusainiwa. Mikataba hiyo ni ushirikiano katika
kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la
Kikagati/Murongo na huduma za usafiri wa anga.
Mikataba minne iliyosalia ambayo inahusu ushirikiano katika usafiri wa
reli, usafiri wa majini; utangazaji na ulinzi wa raia itasainiwa wakati wa
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika
hivi karibuni hapa nchini.
Waziri Mahiga alieleza kuwa kusainiwa kwa mikataba hiyo ni muhimu kwa
kuwa itaimarisha zaidi misingi ya mahusiano yetu, hivyo alizihimiza pande zote
kukamilisha mashauriano hayo ili mikataba hiyo iweze kusainiwa katika muda
uliopangwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa
alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Uganda kufanya kazi kwa pamoja ili kuinua
uchumi kwa madhumuni ya kuwaondolea umasikini wananchi.
Alisema mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka
Uganda hadi Tanzania ni moja ya miradi itakayosaidia kuboresha maisha ya
wananchi, hivyo alisisitiza umuhimu wa kukamilisha taratibu zote zilizosalia
ili ujenzi huo uweze kuanza.
Alihitimisha hotuba yake kwa kuzipongeza Tanzania na Uganda kwa
kufanikisha uwekaji saini wa mikataba miwili ukiwemo wa kuendeleza mradi wa
Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo ambao ulikuwa
katika majadiliano kwa zaidi ya miaka minane.
Kikao hicho cha JPC kimefanyika kufuatia maelekezo
ya Marais wa nchi hizo waliyoyatoa wakati wa ziara ya Rais wa Uganda nchini
mwezi Februari 2017. Viongozi hao waliagiza kikao cha JPC kifanyike kabla ya
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao ulipangwa
kufanyika jijini Dar Es Salaam tarehe 06 Aprili 2017.
No comments:
Post a Comment