Ubora
na thamani ya lugha ya Kiswahili duniani unadhihirika kwa kukubalika
kwake, hali hii inayopelekea lugha adhimu ya Kiswahili kuendelea
kukua na kutumika katika nchi mbalimbali duniani kijamii, kiuchumi na hasa
kibiashara na ushirikiano wa kimataifa.
Mchango
wa lugha hii inaipa hadhi kubwa nchi yetu ambayo ni kitovu cha lugha hii
inayotumika kama lugha rasmi ya mawasiliano katika nyanja mbalimbali na pia
ndiyo lugha unganishi inayotumiwa na watu wengi nchini.
Kihistoria,
lugha ya Kiswahili imekuwa na mchango mkubwa kutokana na kutumika katika
harakati za ukombozi na pia kuwaunganisha Watanzania na kuwafanya
wawe wamoja.
Mara
baada ya Uhuru Tanzania ilianzisha Baraza la Kiswahili (BAKITA) na kupewa
jukumu la kuimarisha na kueneza lugha hii , pia kuhakikisha inatumika kwa
ufasaha pamoja na kukuza msamiati wake ili iweze kukidhi matumizi yake.
Mwaka
1968, lugha hii ilianza kutumika kufundishia katika shule za msingi
hapa nchini. Hatua hii ilimaanisha kila mwanafunzi wa shule ya msingi kuifahamu
vizuri kwa kuiandika, kuisoma na kuielewa.
Aidha,
historia ya kuikuza na kuieneza lugha hii imeanzia mbali, mwaka 1962 hayati
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliitumia kuhutubia Bunge la Tanganyika,
baada ya utawala wake, Rais aliyemfuatia, Ali Hassan Mwinyi aliendeleza
matumizi ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za mawasiliano.
Naye
Rais wa Awamu ya Tatu, Mhe.Benjamin Mkapa na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete walifanikisha maendeleo ya lugha hii kwa kuhimiza matumizi
fasaha katika nyanja za elimu, shughuli zote za Serikali, katika shughuli au
mikusanyiko rasmi pamoja na matumizi mengine ya mawasiliano.
Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam hakikuwa nyuma katika kuhakikisha kinakuza, kinaeneza
na kinakifanya Kiswahili kitambulike zaidi duniani.Miongoni mwa jitihada hizi
ni pamoja na kuanza kutumia Kiswahili kama lugha rasmi ya mawasiliano chuoni
hapo ili kuipa msukumo kwa wananchi wa mataifa mengine yanayohitaji kujifunza
lugha hii.
Katika
kutambua juhudi hizi za Chuo, Balozi wa kwanza wa Kiswahili Barani Afrika, Mama
Salma Kikwete, hivi karibuni alimkabidhi tuzo ya Kiswahili Makamu
Mkuu wa Chuo hicho Profesa Rwekaza Mkandara, ikiwa ni utambuzi wa mchango
wake kwa kurasimisha lugha hiyo kutumika katika shughuli
zote za Chuo na kitaaluma ikiwemo mikutano ya Baraza la chuo.
Aidha,
Mama Salma alitoa wito kwa taasisi mbalimbali kuwekeza katika kuendeleza lugha
Kiswahili ili kuieneza kibiashara ndani na nje ya Bara la Afrika.
Kutokana
na umuhimu wake katika mawasiliano hivi karibuni Bunge la Shirikisho la Jumuiya
ya Afrika Mashariki limeidhinisha lugha Kiswahili itumike katika mikutano yake
ya Bunge.
Bunge
hilo linajumuisha Wabunge kutoka katika nchi sita za jumuiya hiyo ambazo ni
Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini zimepitisha lugha
hiyo kutumika katika nchi zao. Hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kukipaisha
Kiswahili kimataifa.
Ni
kutokana na muktadha huo, baadhi ya wataalamu wa lugha wameishauri Serikali
kuanzisha kozi ya ukalimani katika vyuo vyake ili kuongeza idadi ya wakalimani
hapa nchini hatua ambayo itawaongezea ajira wahitimu wa kozi hiyo.
Hadi
sasa inakadiriwa kuwa idadi ya wakalimani nchini haizidi 20 mbao ndio wanaotoa
huduma katika mikutano mbalimbali ya kimataifa.
Akizungumza
jijini Dar es Saaam hivi karibuni Katibu Mkuu wa Baraza la Kiswahili (BAKITA),
Dkt. Selemani Sewangi alisema kuwa huu ni wakati muafaka kwa Tanzania kuanzisha
kozi hiyo ili kupata wakalimani wa kutosha na wenye weledi, uwezo na maarifa
katika kukalimani lugha ya Kiswahili kwenda lugha nyingine mbalimbali duniani.
Aliendelea
kusema kuwa Tanzania haina kozi hiyo nyuoni, hivyo uwepo wa wataalamu hao hasa
kipindi hiki ambacho nchi inapokuwa kiuchumi kwa kasi, kazi hiyo itoe mchngo
wake ikizingatiwa sekta ya utalii inaendelea kuimarika na kuwa na ongezeko la
wageni mbalimbali wakiwemo watalii, wawekezaji na wengine hatua ambayo itakuwa
fursa ya kutangaza utajiri na maliasili zilizoko nchini mwetu.
“Kuwa
kuna baadhi ya watu ambao wanatafsiri lugha ya Kiswahili wakidhani wanafanya
taaluma ya ukalimani, jambo ambalo si sahihi kitaaluma, watu hawa hawawezi
kupata ajira kutokana na kukosa vigezo vya elimu rasmi ya ukalimani” alisema
Dkt. Sewangi.
Akifafanua
juu ya maana hasa ya ukalimani Dkt. Sewangi alisema kuna
mkanganyiko kati ya kutafsiri na kukalimani, ambapo alisema kuwa
kutafsiri kunaweza kufanywa na mtu yoyote, lakini kukalimani ni lazima mtu
asomee kozi maalumu ili aweze kutambulika kimataifa.
Katika
kuonyesha msisistizo wa kuhakikisha kuwa Kiswahili kinapaa kimataifa, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa
Kiswahili ni lugha ya Waafrika na inazungumzwa katika nchi nyingi na
imekubalika kutumika katika mikutano ya Umoja wa Afrika, hivyo aliwashauri
Watanzania kuipenda lugha hiyo.
Hivi
karibuni Tanzania ilitembelewa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Haile Mariam
Dessalegn ambapo alisema kuwa nchi yake imekubali kuchagua Chuo Kikuu kimoja
ili lugha ya Kiswahili ifundishwe nchini mwake kwa kuendelea kuimarisha
uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Aidha,
Rais Dkt. Magufuli aliahidi kupeleka wataalamu wa lugha ya Kiswahili ili
wafundishe katika chuo kitakachoteuliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia kufundisha
lugha hiyo.
Kwa
kuzingatia umuhimu wa lugha ya Kiswahili huu ni wakati muafaka kwa watunga
Sera, Mamlaka husika na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuanzisha kozi ya
ukalimani katika vyuo vyetu ili wahitimu wapate fursa za ajira katika nchi
mbalimbali na hivyo kuzidi kuipa hadhi na kuieneza lugha ya
Kiswahili ambayo inakisiwa kuwa ni lugha ya 10 miongoni mwa lugha 600
zinazozungumzwa duniani.
No comments:
Post a Comment