Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kiwango cha matumizi ya nishati ya
umeme nchini kimeongezeka na kwamba kwa sasa wanaopata fursa ya kutumia nchi
nzima ni asilimia 67.75 ambapo maeneo ya vijijini wanaopata fursa hiyo ni 49.5%
wakati mijini ikiwa ni 97%.
Profesa Muhongo ameyasema hayo leo jijini Dar
es Salaam, katika uzinduzi wa Jukwaa la Nishati Tanzania, ambalo ni matokeo ya
mradi wa Tanzania na Uholanzi wa kujenga uwezo katika masuala ya nishati
(TDCEB).
“Bara la Afrika watu
wasiopata nishati ni 46%. Kwa mujibu wa tafiti iliyofanyika mwezi Disemba 2016
nchini, inaonyesha Vijijini wanaopata fursa ya kutumia nishati ya umeme
ni 49.5%,, miji yetu yote fursa ya kupata umeme ni 97.3% na kwamba nchi
nzima fursa ya kutumia umeme ni 67.5%, hicho ni kiwango cha kimataifa,
mpango wa nishati vijijini na mijini umefanikiwa kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Hali kadhalika amesema kuwa, tangu mradi wa
matumizi bora ya umeme uanzishwe, serikali imefanikiwa kudhibiti upotevu wa
umeme unaozalishwa kutoka 25% mwaka 2010 hadi kufikia 19%.
“Matumizi bora ya umeme ni
muhimu wakati tulikuwa tunasafirisha umeme mwaka 2010 tulikuwa tunapoteza umeme
25% sasa hivi kwa ajili ya miradi ya matumizi bora ya umeme na uboreshaji wa
nyaya kwa kuweka nyaya zilizo bora na transfoma nzuri sasa hivi upotevu wa
umeme ni asilimia 19 kwa hiyo ndio maana hiki ni kitu muhimu sababu mnaweza
zalisha umeme mwingi lakini unapotea,” amesema.
Kwa upande wa Jukwaa la Nishati, Profesa
Muhongo amesema litasaidia uboreshaji wa sera za nishati pamoja na kuongeza
wataalamu kwenye sekta ya nishati hasa madini na gesi asilia.
“Jukwaa la nishati
limeanzishwa na vyuo vitatu kikiongozwa na UDSM na DIT na Uholanzi kuna vyuo
vitatu na kwamba vitashirikiana kupata wataalamu na waalimu wa vyuo, watu wetu
watatumia hili jukwaa kwenda kujielemisha masuala ya nishati, vyuo vitawezeshwa
kupata vitendea kazi vya kisasa,pia litasaidia kutufanikishia sera ya nishati
sababu hili jukwaa malengo yake ni yaleyale ya maendeleo ya milenia,” amesema na kuongeza.
“Malengo yao ifikapo 2030
watanzania wote na watu wengine wote duniani waweze kutumia nishati kwamba tuwe
na umeme mwingi wa uhakika unaotabiriaka.”
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Florens Luoga amesema jukwaa hilo litasaidia kufanikisha azma
ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kutokana kwamba jukwaa
hilo litawezesha upatikanaji wa wataalamu wa nishati hasa ya gesi na mafuta
ambayo ni sekta nyeti na muhimu katika ukuaji wa sekta ya viwanda.
Kwa upande wa Balozi wa Uholanzi nchini, Jaap
Frederiks amesema “Maendeleo ni kuhusu
uwekezaji kwa watu kwa kutoa elimu kupitia taasisi na vyuo, hili suala ni
muhimu hasa katika sekta ya gesi hususan kipindi hiki ambacho Tanzania
imegundulika kuwa na gesi, na kwamba sekta hii hapo baadae itasaidia kuvutia
sekta binafsi kutumia rasilimali ya gesi na kuleta manufaa kwa watanzania
kupitia fursa za ajira.”
No comments:
Post a Comment