Kwa mujibu wa sheria ya
usajili wa ardhi sura ya 334 ipo aina ya mikataba ya
pango ambayo baada ya kuwa imeingiwa kati ya mpangaji na mwenye
nyumba/eneo ni lazima isajiliwe. Mikataba ya aina
hiyo isiposajiliwa inakuwa haijakidhi
vigezo vya kisheria na hivyo kubatilika.
Aidha pango huhusisha
shughuli mbalimbali. Yapo mapango kwa ajili
ya biashara maduka, bar, mahoteli n.k. na
pia yapo mapango kwa ajili ya makazi.
Iwe umepanga kwa ajili ya biashara au
makazi madhali aina yako ya upangaji inahitaji
kusajiliwa kisheria basi huna budi kufanya
hivyo ili uhalali wa pango lako upatikane.
Kabla ya kuona aina ya mikataba
ya pango ambayo ni lazima kusajiliwa ni vyema kujikumbusha kidogo kuhusu
haki za mpangaji.
1.
HAKI ZA MPANGAJI.
(a) Haki ya kutoingiliwa na mwenye
nyumba ili kumpa uhuru mpangaji kufurahia pango lake.
(b) Haki ya
kumpa taarifa(notice) mapema mpangaji ikiwa mwenye
nyumba anataka kukagua nyumba/eneo lake.
(c) Haki ya kutoondolewa
au kusitishiwa mkataba mpaka baada ya
kupewa taarifa maalum( notice) .
(d) Haki ya
kuambiwa ukweli kuhusu hali ya nyumba kabla
ya kusaini mkataba wa pango. Mfano kuambiwa
ikiwa eneo linajaa maji kipindi cha mvua,
kuambiwa ikiwa nyumba inavuja n.k.
(e) Haki ya kukataa sharti lolote ambalo linalenga
kuminya uhuru wa mpangaji au linalovunja sheria yoyote ya Tanzania.
(f) Haki ya kupewa taarifa
mapema (notice) kabla ya kupandisha kodi ya pango.
(g) Haki ya kupewa
taarifa mapema (notice) kabla ya kubadilisha sharti lolote katika mkataba wa
pango.
Haki ni nyingi
hizi ni baadhi tu.
2.
MKATABA WA PANGO AMBAO NI LAZIMA KUSAJILIWA
Kifungu cha 54 (1) cha Sheria ya
Usajili wa Ardhi, Sura ya 334 kinasema kuwa pango ambalo mkataba wake
unazidi miaka mitano linatakiwa kusajiliwa.
Wapo watu wanapanga mahoteli, bar,
maduka nk. ambao miaka ya pango katika makubaliano yao ni zaidi ya
mitano. Hawa mikataba yao ni lazima isajiliwe.
Mara nyingi mkataba wa pango huweza kuwa wa
miaka mingi kutokana na aina ya biashara anayotaka kufanya mpangaji halikadhalika uwekezaji anaotarajia kufanya eneo analotegemea kupanga. Wakati mwingine
mpangaji hukubaliana na mwenye eneo kufanya marekebisho makubwa (renovation) ili eneo lifanane na aina ya biashara anayotaka kufanya.
Mbali na hayo ni vema kufahamu pia kuwa
mkataba ambao ni chini ya miaka mitano lakini mkataba huo una
sharti la kuhuisha (renew) kwa miaka mingine, ambapo ukijumlisha
miaka ya awali na hiyo ya kurenew jumla inazidi mitano basi nayo ni
lazima kusajiliwa.
Tumeongelea mikataba
inayozidi mikaka mitano lakini hatupaswi kusahau
kuwa hata mikataba ya pango iliyo chini ya miaka mitano inaweza kusajiliwa
japo sio lazima. Mikataba hii una chaguo kusajili au kutosajili. Kisheria
kutosajiliwa kwake kwa namna yoyote hakuathiri uhalali wake.
3. WAPI UKASAJILI.
Msajili wa nyaraka
anayepatikana ofisi za ardhi ndiye
anayehusika na usajili wa mikataba hii. Unapofika
ofisi yoyote ya ardhi utapewa maelekezo lipi la kufanya ili
mkataba wako uweze kusajiliwa.
Aidha ipo ada ya kulipa kabla ya usajili
ikiwemo kodi ya faida.
No comments:
Post a Comment