Benki ya
Exim Tanzania imetoa msaada wa madawati 50 yenye thamani ya milioni tano kwa
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, madawati ambayo yatagawanywa kwa Shule
ya Msingi Kisitwi na Chajware zilizopo wilayani humo.
Akizungumza wakati wa
hafla ya kukabidhi madawati hayo, Meneja wa Exim Bank mkoani Morogoro, Patrick
Njole alisema msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika
kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Exim Bank inapongeza jitihada ambazo zinafanywa na serikali
za kuweka mazingira bora ya kujifunza na kwa kutoa msaada huu kwa shule za
Morogoro, tunaamini itakuwa mwanzo wa kuelekea mbele zaidi kusaidia maeneo
mengine nje ya miji mikubwa na kuyafikia maeneo ya vijijini,” alisema Njole.
Njole alisema wamekuwa
wakiwekeza kwa muda mrefu katika sekta ya elimu na kuahidi kuwa benki ya Exim
itaendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kusaidia kuboresha mazingira
bora ya elimu ya Tanzania.
Nae Mkuu wa Wilaya ya
Gairo, Siriel Mchembe aliishukuru benki ya Exim kwa msaada ambao wamewapatia
kwa ajili ya kusaidia kupunguza changamoto ya uchache wa madawati unaowakabili
katika mkoa wa Morogoro.
“Madawati ambayo mmetusaidia yatatusaidia kupunguza uhaba wa
madawati ambao unatukabili katika shule zetu. Tunawaomba wadau wengine kufanya
kama Exim Bank kusaidia mikoa ambayo bado ina tatizo hili,” alisema
Mchembe.
Mkuu
wa wilaya ya Gairo, Bi Siriel Shaidi Mchembe akipokea madawati 50 yenye thamani
ya shs milioni tano kutoka kwa Meneja Masoko wa Benki ya EXIM Tanzania Bw
Abdulrahman Nkondo kama msaada kwenda kwa shule ya Kisitwi na Chakware za
Mkoani Morogoro.
Mkuu
wa wilaya ya Gairo, Bi Siriel Shaidi Mchembe akiwa ameketi na baadhi ya
wanafunzi wa shule ya msingi Kisitwi wakati wa sherehe za makabidhiano ya
madawati 50 kutoka kwa Benki ya EXIM Tanzania. Madawati yenye thamani ya shs
milioni 5 yatagawanywa kati ya shule mbili; Kisitwi na Chakware za mkoani
morogoro. Kulia ni Meneja Masoko wa Benki ya EXIM Tanzania Bw Abdulrahman
Nkondo na kushoto ni Meneja wa Tawi la Benki hiyo Mkoani Morogoro Bw Patrick G
Njole.
No comments:
Post a Comment