Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya CORE Capital Limited ambayo ndio iliyobuni mfuko huo, Bw George
Fumbuka (katikati) akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo
mpango-mkakati unaoendeshwa na kampuni hiyo kupitia Mfuko wa uwekezaji wa
pamoja wa UMANDE UNIT TRUST (UUT) utakaowawezesha wawekezaji wadogo na wale
wenye kipato cha chini na cha kati waweze kununua hisa za kampuni ya Vodacom
Tanzania kwa kupitia njia ya vipande. Wengine ni Meneja wa Mfuko huo Bi Sandra
Felician na Naibu wake Bi Nkunde Shoo
MFUKO wa uwekezaji wa pamoja wa UMANDE UNIT TRUST
(UUT) leo umezindua rasmi mpango-mkakati wake wa kifedha utakaowawezesha
wawekezaji wadogo na wale wenye kipato cha chini na cha kati waweze kununua
hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kupitia njia ya vipande.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CORE Capital Limited ambayo ndio
iliyobuni mfuko huo, Bw George Fumbuka alisema kiwango cha chini cha
ununuzi wa hisa za Vodacom ni 85,000/= (hisa 100 kwa 850/= kila hisa), kwa
mkupuo kinaweza kuwa kiasi kikubwa kwa wawekezaji wadogo wadogo, wa kipato cha
chini.
“Mantiki ya mkakati huu ni kuwakusanya pamoja wale
wote wenye mitaji midogo ili waweze kwa pamoja kufikia viwango vinavyohitajika
katika ununuzi wa hisa za VODACOM. Kima cha chini ni shilingi 13,500 tu, yaani
vipande 100 vya shilingi 135/= kila kimoja. Dhana hii si mpya kwa Watanzania; mara
nyingi tu hutumika kwenye shughuli za pamoja, huitwa “UMOJA NI
NGUVU.’’ Alisema
Alisema mpango huo pia utatoa fursa kwa wawekezaji
wa kigeni wakiwemo watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) kuweza kunufaika
na hatua hiyo ya serikali kwa kuwa uuzwaji wa hisa hizo kupitia soko la Hisa la
Dar es Salaam (DSE) hautoi fursa kwa wawekezaji wa kigeni.
“Kwa kuwa mauzo ya hisa hizo hapa nchini
hayahusishi wawekezaji wa kigeni wakiwemo watanzania wanaoishi nje yaani
Diaspora, milango ipo wazi kwao kupitia mfuko wa uwekezaji mtaji wa Umande
(Umande’s capitalisation fund),utakaowawesha kununua vipande badala ya wao
kwenda moja kwa moja kwenye soko la hisa,’’ alisema.
Zaidi Bw Fumbuka aliwahakikishia walengwa wa mpango
huo kuhusiana na uhakika wa wao kujipatia gawio na faida zitokanazo na mtaji
(dividends and capital gains) kama kawaida kwa kuwa thamani ya vipande
itakwenda sambamba na thamani ya hisa za kampuni hiyo ya huduma za simu za
mkononi.
“Mpango mkakati huu una baraka zote za Kampuni ya
Vodacom na za Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) chini ya Kanuni za Mifuko ya
Uwekezaji ya mwaka 1997.” Alibainisha.
Hata hivyo alifafanua kwamba watakaopitia mkakati
huo, wawe ni wawekezaji wadogo wadogo au wale wa nje, hawataweza kumiliki hisa
za VODACOM moja kwa moja; badala yake watamiliki vipande vya Mfuko
utakaopatikana kwa michango yao.
“Kwa maana hiyo Mfuko wa
UUT ndiyo utanunua hisa za VODACOM kwa niaba yao na watafaidi matunda ya
uwekezaji kwa njia hiyo. ‘’ alisema huku akiongeza kuwa Vipande vitanunuliwa
kwa njia ya simu tu: *150*36#, huku kima cha chini kikiwa ni Tsh 13,500/=.
No comments:
Post a Comment