Kilimanjaro 22 Februari 2025: Serikali mkoani hapa imeipongeza kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania kwa kazi kubwa ambayo inafanya kwa kupanda miti pamoja na shughuli zingine zinahusiana na uhifadhi wa mazingira.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu wakati wa hafla ya kampeni ya kupanda miti iliyofanyika kata ya Kimochi, wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, mwishoni mwa wiki.
Katika risala iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Moshi Bw. Godfrey Mnzava, Bw Babu alisema kuwa kampeni ya upandaji miti iliyofanywa na kampuni hiyo haina budi kuwa endelevu ili kuendelea kulinda mazingira na uhifadhi wake kwa ujumla.

“Niwapongeze Yas na wadau wengine walioshirikiana nao kwa kazi nzuri hii haswa ikitiliwa maanani ya kuwa changamoto kubwa inayoikabili dunia ni mabadiliko ya tabia nchi ambayo njia pekee ya kukabiliana nayo ni upandaji wa miti kwa wingi na kuhifadhi mazingira”, alisema.
Aliongeza, “Tunahitaji kuwa na mazingira mazuri maana tunayategemea kwa shughuli zetu za kila siku ikiwemo upatikanaji wa rasilimali nyingi ambazo tunahitaji kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali muhimu kwa binadamu; hatuwezi kukwepa wajibu wa kuyatunza mazingira kutokana na umuhimu wake huo”.
Alisema kuwa ni jukumu la kila taasisi na mtu mmoja mmoja ni kuhakikisha kuwa miti inapandwa kwa wingi wakati huo huo kuhakikisha kuwa inatunzwa na kukua kutokana na ukweli kuwa mazingira yakiharibika na maisha ya wanadamu yatakuwa magumu.
“Nichukue fursa hii kuendelea kuwasihi viongozi wetu wa kidini kuendelea kuungana na Serikali katika kuwahamasisha watu kuendelea kupanda miti na pia kuhakikisha wanayatunza mazingira ili taifa liendelee kuwa mahali salama pa kuishi”,alisema.
Akiongea katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Yas, Bw. Innocent Rwetabura, alisema kampuni hiyo imelenga kupanda zaidi ya miti 25,000 kwa mwaka wa 2025, kupitia kampeni iliyobeba kaulimbiu Green for Kili, Hatua Moja Mti Mmoja.
Alisema kampeni hiyo imelenga kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla ikiwemo kuhakikisha kila halmashauri inapanda miti milioni 1.5 kwa mwaka.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wadau wengine ambao wanaungana na sisi katika kampeni hii, ambao nia pamoja na WWF, Pangani Basin Water Board (PBWB), hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (MDC)”, alisema.
Kwa upande wake mwakilishi wa WWF katika hafla hiyo, Bi. Joan Itanisa alisema taasisi hiyo imeendelea kuungana na wadau wengine wa mazingira katika kuhakikisha pamoja na mambo mengine uoto wa asili unarudi.
“Takwimu zinazotolewa na wataalam mbalimbali wa mabadiliko ya tabia nchi na mazingira zinaonyesha ni namna gani hali ya ikolojia ya Mlima Kilimanjaro inavyozidi kudhoofu; ndiyo maana WWF tumekua tukifanya kazi kwa muda sasa kunusuru ikolojia hii muhimu kabisa kwa nchi yetu na afrika kwa ujumla”, alisema.
Naye mwakilishi wa KINAPA, Bw. Mdesa Mapinduzi aliipongeza kampuni ya Yas kwa juhudi inazofanya kuhakikisha mazingira haswa yanayozunguka Mlima Kilimanjaro yanaendelea kuwa mazuri.
“Katika ushirikiano huo, umetuwezesha KINAPA kupanda miti zaidi ya 30,000 na pia kuanzisha vitalu vya miche ya miti, tayari tuna zaidi ya miche 200,000 kwenye vitalu hivyo”, alisema.
Mwakilishi kutoka PBWB Bi Arafa Majid, alisema kuwa taasisi hiyo inasimamia jumla ya vyanzo vya maji 762 vilivyoko mkoani Kilimanjaro na ambavyo alisema kuwa vyote vinahitaji kuhifadhiwa ili kupatikane maji ya uhakika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya binadamu.
“Chanzo hiki kilichoko hapa Kimochi ni moja wapo ya vyanzo hivyo na leo hii tutapanda miti 200 kwa ajili ya kukihifadhi, hii ni hatua nzuri ambayo hatuna budi kuwashukuru Yas Tanzania kwa kuja na kampeni hii”, alisema.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (MDC) Bw. Shadrack Mhagama, alitoa rai kwa wananchi kuacha kukata miti kiholela na kwamba kama kuna ulazima wa kufanya hivyo wahusika hawana budi kufuata taratibu zilizoko kabla ya kufanya hivyo.
“Hata kama mti umeupanda wewe, ni lazima upate kibali kutoka Serikalini ambacho hutolewa na Mkuu wa Wilaya tu, fuata taratibu zilizoko na kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo utapata kibali kutoka kwa mamlaka husika kukata mti huo”, alisema.
No comments:
Post a Comment