HERI YA MWAKA MPYA 2017 siku hii ni siku maarufu sana duniani ambayo wengi huiona ni neema kuifikia.
Neema hiyo huzingatia hali halisi malengo na mikakati ambayo wengi hujiwekea, lakini wengine wakashindwa kuifikia kutokana na kukutwa na mauti. Unapofika mwaka mpya, wengi hushukuru kwa namna tofauti. Wapo ambao huenda nyumba za ibada kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuingia mwaka mpya. Baadhi ya madhehebu hufanya ibada ya mkesha ama kwenye nyumba za ibada au kwenye maeneo ya wazi lengo likiwa ni kumshukuru Mungu kwa kufika siku hiyo.
Kwa hiyo, Januari mosi inasubiriwa kwa hamu siyo tu kusherehekea ushindi wa kuuona mwaka mpya, bali pia kwa ajili ya kuweka mipango baada ya tathmini ya mwaka uliomalizika. Ingawa baadhi ya jamii na hata dini mbalimbali, zina maadhimisho yao ya mwaka mpya, kwa upande wa Januari mosi, imekuwa kiunganishi kwa watu wote bila kujali tofauti za kiimani kutokana na kuadhimishwa na kusherehekewa na watu mbalimbali kwa namna tofauti.
Mwaka mpya wa kiislamu Mwaka huu wa Kiislam ambao unafupishwa kama H au Hijriyyah, tarehe 1 Muharram H ilikuwa ni sawa na tarehe 16 Julai 622 M. Na ndivyo hivi inavyohesabika mpaka leo. Historia inasema miaka ya kiislamu imeanza kuhesabika baada ya Maswahaba kuhama kutoka Makkah kwenda Madiynah.
Umar alitoa ushauri kuwa kwa vile ni mara ya kwanza wanahamia katika mji ambao wataanza kutekeleza sharia ya Kiislam, basi ni bora kuanza kuhesabu miaka kwa kuanzia mwezi huo waliohajiri, ambao ulikuwa ni mwezi wa Muharram. Na pia inasemekana kuwa ‘Umar alikuwa akipata barua kutoka kwa magavana wa nchi mbalimbali zilizokuwa chini ya Uislamu, na zilikuwa zikiandikwa majina ya miezi bila tarehe.
Akawashauri Maswahaba wenzake kuwa kuweko na tarehe. Wako waliopendekeza tarehe zianze kwa kufuata miaka ya Kirumi, na wako waliopendekeza zianze kwa miaka ya kifursi. Mwishowe wakakubaliana ianze pale alipohamia Nabiy Madiynah.Maadhimisho ya mwaka wa kiislamu yamekuwa yakifanyika kwa namna mbalimbali hususani katika nyumba za ibada kwa kufanya swala na kuwapo mawaidha.
Mathalani, mwaka huu, madhehebu ya Bohora, yaliadhimisha kupitia tamasha kubwa lililofanyika jijini Dar es Salaam. Maadhimisho yalianza Oktoba 2 hadi Oktoba 11. Maadhimisho hayo yaliwaleta nchini wafuasi zaidi ya 30,000 kutoka nchi mbalimbali duniani na kuongozwa na Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Bohora Duniani Mtukufu Dk Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb (TUS).
Rais John Magufuli, aliyealikwa, aliwapongeza viongozi na wafuasi wa madhehebu ya Bohora kwa kutumia maadhimisho haya kuhimiza amani, upendo na mshikamano. Kalenda ya Kichina Wachina husherehekea mwaka mpya wa kalenda yao kama desturi. Mwaka mpya hutokea kati ya Januari 21 na Februari 21. Kalenda ya Kichina ni kalenda ya kidesturi inayoitwa pia kalenda ya Han.
Kalenda wa Kichina inafuata mwendo wa mwezi pamoja na mwendo wa jua kwa hiyo inaunganisha tabia za kalenda ya mwezi na kalenda ya jua. Sherehe za mwaka wa kichina, hupewa kipaumbele na zinatambuliwa kuwa wakati maalumu wa mapumziko ya kazi. Inaelezwa kwamba, hadi sasa sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa kichina imekuwa ikiadhimishwa kwa miaka 4,000 nchini China, lakini mwanzoni sikukuu hiyo haikuwa na tarehe maalumu.
Hadi miaka elfu mbili na mia moja iliyopita wahenga wa China walihesabu mwaka kwa mzunguko kamili wa sayari ya Jupita, sikukuu hiyo iliitwa sikukuu ya Jupita, ilipofika miaka elfu moja iliyopita ndipo Wachina walipoanza kuiita siku hiyo sikukuu ya Spring. Hata hivyo, mipango yao ya nchi huzingatia kalenda ya Gregory; inayoanza Januari Mosi. Licha ya China, pia Vietnam mwaka wao husherehekewa kati ya Januari 20 na Februari 20.
Cambodia Wa Cambodia husherehekea mwaka wao Aprili 13 au Aprili 14 na hujulikana kwa jina la asili kama Songkran. Jamii huwa na siku tatu za maadhimisho, ya kwanza inaitwa “Moha Songkran”, ya pili “Virak Wanabat” nay a mwisho ni “Virak Loeurng Sak”. Wakati wa kipindi hiki cha maadhimisho, husherehekea kwa kucheza michezo ya aslili. Januari mosi Januari Mosi ambayo imekuwa kiunganishi kwa jamii mbalimbali duniani, inamulikwa kuanzia enzi za wafalme mbalimbali wa Kirumi.
Walifikiria kuadhimisha siku maalumu ambayo ni lazima iendane na siku ya mwanzo na mwisho wa mwaka. Inaelezwa kwamba, mwanzo kabisa, sherehe za Mwaka Mpya zilishuhudiwa kwa mara ya kwanza huko Mesopotamia karibu miaka 2000 iliyopita. Ilisherehekewa na Wamisri, Waajemi na Wafoeniki wakati wa Equinox ambao ni katikati ya mwezi Machi na Wayunani walisherehekea katika kipindi cha majira ya baridi. Kalenda ya kale ya Kirumi ilionesha kwamba, Mwaka Mpya uliangukia Machi Mosi.
Kalenda hii ilikuwa na miezi 10 tu na Machi ilikuwa mwezi wa kwanza wa mwaka. Asili ya kalenda hii ni mzunguko wa mwezi, ikianzia majira ya kuchipua na kumalizia na majira ya vuli. Mfalme wa pili wa Roma ndiye aliyeugawa mwaka katika miezi 12 ya mzunguko wa jua na kuongeza miezi ya Januari na Februari. Mwaka mpya ukabadilishwa na kuwa Januari kutokana na mwezi huo kusadifu mwanzo wa miaka ya kiraia katika Roma. Lakini jambo hili halikukubaliwa kikamilifu na watu wa Roma kwani waliendelea kuadhimisha mwezi wa Machi tu.
Mwaka 46 KK, Kaizari wa Roma, Julius Caesar ndiye alitangaza rasmi kuwa Januari Mosi ndio mwaka mpya. Wakati huo Warumi walikuwa wakimuabudu mungu Janus anayeelezewa kuwa alikuwa na nyuso mbili; moja ikiangalia mbele na nyingine ikiangalia nyuma. Mwezi wa Januari ulipewa jina la mungu huyo wa Kirumi. Hatimaye, kaisari alipata wazo la kuanzisha Januari kama mwanzo wa mwaka mpya.
Inasemekana kuwa Kaisari aliisherehekea Januari mosi kama mwaka mpya kwa kuamuru majeshi ya mapinduzi ya Wayahudi kurudi nyuma. Waliadhimisha mwanzo wa mwaka kwa kurejesha sheria za zamani kabla ya amani kuenea. Watu wakajua kuwa Januari ndiyo mwezi wa kwanza wa mwaka.
Takriban miaka 500 baadaye, Papa Gregory XIII alipiga marufuku kalenda ya zamani ya Julian na kuanzisha kalenda ya Gregori ambayo ilijumuisha mwaka mrefu wenye siku 366 ambao mwezi wa Februari unakuwa na siku 29 baada ya kila miaka minne ili kudumisha uwiano kati ya misimu na kalenda. Mnamo mwaka 1582, kalenda ya Gregori ilianzishwa kusherehekea mwaka mpya katika siku ya kwanza ya Januari. Makala haya yamendaliwa kutokana na vyanzo mbalimbali kutoka kwenye mtandao wa intaneti.
No comments:
Post a Comment