WANASOKA WAFIKIRIE ZAIDI YA NYUMBA NA GARI - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Sunday, January 1, 2017

WANASOKA WAFIKIRIE ZAIDI YA NYUMBA NA GARI


KUANZIA mwishoni mwa miaka ya sabini hadi mwanzoni mwa miaka ya tisini tasnia ya soka Tanzania haikuwa na heshima na thamani iliyopo sasa.

Ingawa inaaminika kwamba katika miaka hiyo Tanzania ilikuwa na wachezaji soka wengi wenye talanta za hali ya juu sana ukilinganisha na sasa kwa vigezo ambavyo wasemaji wanaviamini. Katika nyakati hizo hapo wachezaji wengi walidumu kwenye timu zao kwa kipindi kirefu tena wakicheza soka ya hali ya juu kwa mapenzi yote.
Shida ilikuwa kwamba soka haikuwa na heshima iliyoanza kujengeka katika jamii yetu kuanzia mwishoni mwa miaka ya tisini hadi sasa, na kuonekana kwamba soka ni kazi kama zilivyo kazi zingine katika jamii, tena yenye malipo zaidi ya hizo ambazo watu wameingia darasani kuzisomea.
Wachezaji soka wa zamani walichukuliwa kama wahuni tu na jamii yetu, hali ambayo iliwaathiri sana wengi wao kwa namna moja au nyingine na kujikuta wakiamini kwamba wao si watu wenye thamani kubwa zaidi ya umaarufu tu na kujikuta wakiathirika kimaisha hadi sasa.
Wengi walijingiza kwenye ulevi na uasherati ambao ulimaliza sana pesa zao kutokana na kukosa elimu ya nidhamu ya matumizi ya pesa.Hii ni kutokana na ukweli kwamba haikuwa ajabu kuona mchezaji soka mwenye talanta kubwa si yule asiyejua kusoma wala kuandika na aliyetoka kwenye familia fukara kupita wenzie.
Hadi leo soka inachezwa sana na watoto kutoka familia za kifukara na wenye nazo utawakuta wanazuga tu wakihangaika zaidi na masomo kutokana na shinikizo za familia zao tajiri Haikuwa ajabu kuona mzazi akimkataza binti yake kuolewa au hata kuwa na uhusiano na mchezaji soka wa miaka ya nyuma kwa kuamini kwamba, mtu huyo ni mhuni ambaye hatakuwa na cha kumpa binti yake na pengine kumsababishia matatizo tu.
Kipindi hicho timu nyingi zilikuwa ni za mashirika ya umma, idara na taasisi za serikali na makampuni makubwa ukiondoa timu mbili kongwe za Simba na Yanga ambazo zilikuwa za wananchi. Wengi ya wachezaji waliokuwa kwenye timu za mashirika ya umma, makampuni, idara na taasisi za serikali walipata bahati ya kupata ajira tena bila kujali wana elimu gani. Wapo ambao hadi leo kupitia soka wamo makazini na ambao hata vifo vimewakuta humo.
Lakini pia wapo ambao baada ya shughuli za kisoka kuisha, aidha timu kuvunjwa au mchezaji kuhama timu, walikosa kazi na kule Simba na Yanga walikokwenda kwa kuwa hakuna kampuni wala shirika, baada ya talanta kupotea nao walipotezwa na wanahaha mitaani na wale ambao Mungu kawachukua, walikufa katika umaskini ulitopea.
Inaaminika kwamba, kutokana na ukweli kuwa, wachezaji wengi wa zamani walikuwa wanacheza kwa mapenzi ya dhati na tangu siku hizo linapokuja suala la ushabiki wa soka hapa Tanzania, ni Simba na Yanga ndio zenye vipaumbele, basi malengo ya wachezaji wengi yalikuwa ni kucheza aidha Yanga au Simba na pengine Taifa Stars tu basi.
Hata kama kulikuwa na wale waliokuwa na viwango na talanta ya kucheza timu za ng’ambo, lakini kwa kuwa walikuwa washafikia malengo yao, hawakuona tena sababu ya kuendelea kujibidisha na kutunza viwango vyao ambavyo vingeweza kuwatoa kimaisha kwa kupata timu nje. Dumu daima mtu anayefikia malengo ni kwamba atakuwa ashafika kileleleni.
Kama ushafika kilele cha kitu chochote, kinachofuata ni kuteremka mtu bila kujali namna utakavyokuwa unateremka kwani hakuna kwa kwenda zaidi. Hapo ndipo ambapo wachezaji wa sasa wanawaita wachezaji wa zamani kwamba wamebugi kwa kuwa malengo yao yalikuwa ni kucheza Simba na Yanga tu tena kwa mapenzi bila hata kujali maslahi. Pale walipopata pesa walifanya matumizi ambayo wao wanayaona wamewafikisha hapo walipo.
Ni kweli soka ya zamani haikuwa na pesa kama sasa, lakini si kweli kusema kwamba wachezaji walikuwa hawapati pesa kabisa, kwani wapo ambao walifanikiwa kujikwamua na sasa wanaishi vyema kwa vijisenti hivyo hivyo. Miaka ya sasa soka imekua ndio habari kubwa nchini na duniani kwa ujumla, wachezaji soka ndio habari ya mjini popote pale uendapo duniani, kwani malipo na mishahara yao ni hatari kubwa.
Hapa nchini kwetu kuna wanasoka wanalipwa pesa nyingi ingawa bado kuna namna ambavyo huwezi kutofautisha sana jinsi ambavyo mchezaji wa sasa na yule wa zamani wanavyoishi kimalengo. Bado wachezaji wa sasa hawana njaa ya kutafuta malisho mazuri nje ya nchi kama ilivyokuwa kwa watangulizi wao pia. Wanaridhika na pesa wanayopata hapa, tena kwa haraka sana na ndio maana wengi wao hawawezi kutunza viwango vyao hata kwa misimu mitano tu mfululizo.
Baadhi wanajiingiza kwenye majanga makubwa makubwa ya utumiaji wa dawa za kulevya, bangi na uesherati kama ilivyokuwa kwa kaka na baba zao. Wakiamini kwamba watangulizi wao walibugi kwa kucheza soka kwa mapenzi, wachezaji wa sasa wanatanguliza pesa kuliko kitu chochote ndio maana sio ajabu kumuona mchezaji wa kariba ya timu ya taifa anaingia kwenye shutuma za kuuza mechi.
Wakati watu wamewahi kuichezea Taifa Stars kwa moyo mmoja wakiwa wanalipwa posho ya Sh 1,000 kwa kutwa, na kamwe hukusikia mtu anagoma kwenda kambini, leo wao wanalipwa Sh 50,000 kama posho kwa kutwa na matukio ya kuikataa timu ya taifa yanazidi kuongezeka kwa kuwa wengi wao wanalipwa mishahara minono na klabu zao. Inaaminika wachezaji wengi wa zamani hawakujenga nyumba na hivyo kukosa mahali pakuishi penye kueleweka, wengi wao wanaonekana walibugi.
Hivyo malengo makuu ya wachezaji wa leo ni kuwa na nyumba na gari, na kila mwenye uwezo wa kupata hivyo hujiona aliyefikia malengo yake na kukosa njaa ya kutafuta maendeleo zaidi. Bahati mbaya sana ni kwamba kwa pesa ambayo ipo kwenye soka la kileo, wachezaji wengi sana ambao wapo kwenye klabu kubwa wamefikia malengo yao kwani karibu nusu yao wanamiliki nyumba na magari tena wana uwezo wa kubadilisha magari kila msimu.
Yule ambaye hana nyumba utasikia tu mtaani ‘akiimbwa’ kwamba hana akili wala malengo kwani hana hata gari wala sehemu ya kuishi wakimaanisha kwamba hajajenga nyumba. Kwa mtindo huu, huwezi kupata mchezaji ambaye utamuona anatunza kiwango chake kwenye aidha klabu au timu ya taifa kwa miaka mitano mfululizo, kwani wengi wanaoitwa huko ni wale ambao wamefikia malengo na wako kileleni sasa wanatafuta namna ya kushuka tu.
Ukifikia malengo yako kila mtu unamuona hana maana kwako, ndio maana vijana leo kwa kuwa ana nyumba na gari, huwezi kumshauri kitu chochote akakuelewa zaidi ya kukudharau na kukuona ulibugi wakati unacheza soka. Ni kweli kila mtu ana malengo yake, lakini ifike hatua tuelezane ukweli kama wana jamii kwamba unaweza ukawa na nyumba na gari, lakini bado muda mfupi mbele ukawa fukara ambaye hata baiskeli wala mkokoteni huna.
Kwani katika maisha ya kawaida ukiwa na miaka 35 wewe ni kijana ambaye hata kupewa ujumbe wa nyumba 10 ni mashaka, lakini katika soka hiyo ni miaka ambayo utaitwa babu na kukutaka uachane na soka.
Kwa kuwa bado wengi wetu hatuna elimu wala nidhamu ya matumizi ya pesa, basi kama Allah atakupa uhai na kukupa miaka mingine 15 nje ya soka atakuwa amekupa mtihani mkubwa sana. Vijana amkeni muangalie mlipo mpambane maisha nje ya soka ni magumu na wala hayawezi kuwa rahisi kwa kumiliki gari na nyumba na simu nzuri, yanataka zaidi ya hapo!

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages