‘UKIWA NA VINASABA VYA SELIMUNDU, TAFUTA MWENZI ASIYE NAVYO’ - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Sunday, January 1, 2017

‘UKIWA NA VINASABA VYA SELIMUNDU, TAFUTA MWENZI ASIYE NAVYO’

SHIRIKISHO la vyama vya Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukizwa (TANCDA) limekuwa katika harakati za kuelimisha umma juu ya namna nzuri ya jamii kuepuka magonjwa hayo.
Miongoni mwa njia ambazo zinatumika, ni pamoja na kutoa machapisho yenye kuelezea dalili, athari na kinga ya magonjwa husika. Katika mwendelezo wa makala zitokanazo na chapisho la shirikisho la ‘Mtindo wa maisha na magonjwa yasiyoambukiza’, leo tunakuelezea kuhusu ugonjwa wa selimundu.
Selimundu ni nini?
Hewa ya oksijeni inasafirishwa ndani ya chembechembe nyekundu za damu ikijishikiza kwenye protini inayoitwa hemoglobini. Pamoja na kushikilia oksijeni, hemoglobini inachangia umbo la chembechembe hizi ambalo kwa kawaida ni bapa na mviringo kama vile sahani. Selimundu ni ugonjwa wa kurithi unaosababisha umbo la chembechembe nyekundu za damu kuwa uliochongoka kama mundu au mwezi mchanga unavyoonekana.
Chembechembe za namna hii zinaishi kwa muda mfupi kuliko chembechembe za kawaida, zinapita kwa shida kwenye mishipa midogo ya damu na wakati mwingine kusababisha kuziba kwa mishipa hiyo na hivyo sehemu husika kukosa damu, hewa na virutubishi.
Urithi wa selimundu
Tabia ya selimundu (AS) haijidhihirishi kama ugonjwa. Umuhimu wake mkubwa ni kwamba mtu anakuwa na uwezo wa kuipitisha tabia hiyo kwa watoto wake. Endapo mwenzi wake pia ana tabia ya selimundu, basi kuna uwezekano wa moja kati ya nne kwa kila ujauzito kuwa jeni ya selimundu itarithiwa kutoka kwa wazazi wote wawili na mtoto atakuwa na ugonjwa wa selimundu (SS), pia ni moja kati ya nne na kuna uwezekano wa wawili kati ya wanne kuwa mtoto atarithi tabia ya selimundu (AS). Ni jambo la muhimu kwa wazazi kupima, ili kufahamu ikiwa mtoto wao ataweza kuathirika.
Urithi wa jeni ya mundu
Kila mtoto hupokea jeni moja ya hemoglobini kutoka kwa kila mzazi. Jeni hizi mbili huamua aina ya hemoglobini. Jeni inayopeleka kuwa na hemoglobini ya kawaida hujulikana kama (A). Jeni inayopelekea uwepo wa ugonjwa wa selimundu hujulikana kama (S). Endapo utarithi jeni mbili za mundu, utakuwa na ugonjwa wa selimundu (SS). Endapo utarithi jeni moja ya mundu, basi utakuwa na hemoglobin ya kawaida (AA).
Asilimia 13 hadi 15 ya watu ncini wana tabia ya selimundu (AS) na inakadiriwa kuwa watoto 8,000 hadi 15,000 wanazaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa selimundu. Umuhimu wa jeni ya selimundu Watu wenye AA wako katika hatari ya kufariki kutokana na malaria. Watu wenye selimundu wako katika hatari kubwa zaidi ya kufariki kutokana na ugonjwa wa malaria na wa selimundu. Watu wenye tabia ya selimundu hukingiwa dhidi ya kupata malaria kali na hatimaye kifo.
Athari za selimundu
Watu wenye ugonjwa huu wako katika hatari ya kufariki mapema kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya yakiwemo malaria, maambukizi ya bakteria na kiharusi. Zaidi ya hapo, wanaweza kuhitaji kubadilisha damu mara kwa mara (hatua ambayo inaongeza uwezekano wa kupata virusi vya Ukimwi na ini) na kupata huduma za afya mara kwa mara hospitali.
Dalili za selimundu
Watu wenye tabia ya selimundu na baadhi ya wale wenye ugonjwa wa selimundu, hawana dalili yoyote. Kwa upande mwingine, baadhi ya watu wenye ugonjwa huathiriwa kwa kiasi kikubwa na huwa na dalili wakati wa utoto wao. Njia pekee ya kuwa na uhakika kuhusu hali yako ya umundu wa hemoglobini ni kufanya kipimo cha damu. Dalili zinazotoka na chembechembe nyekundu za damu kuziba mishipa ya damu na chembechembe hizi kuwa na uhai mfupi kuliko kawaida, ni pamoja na upungufu wa damu (anaemia).
Maumivu makali kwenye mifupa, karibu na viungio na fumbatia; vipindi vya homa vya mara kwa mara kutokana na malaria na maambukizi ya bakteria ni dalili nyingine. Nyingine ni maumivu ya kifua na kukosa pumzi, uvimbe sehemu za tumbo kutokana na kupanuka kwa bandama, vidonda sugu kuzunguka vifundo na muundi. Dalili nyingine ni homa ya manjano inayosababishwa na kuharibika kwa kasi kwa seli nyekundu za damu (sehemu nyeupe ya jicho kuwa ya manjano).
Kuziba kwa mtiririko wa damu ambao husababisha uharibifu wa tishu na tatizo hutegemea sehemu ya mwili iliyoathirika. Kwa mfano, udhaifu wa ghafla au kupoteza hisia, maumivu ya kichwa au kubadilika ghafla kwa uwezo wa kuona. Dalili nyingine ni kuchelewa kukua na kuendelea kimwili. Namna ya kuepuka selimundu Ugonjwa huu hauambukizi na hauna tiba ya moja kwa moja. Kinachotakiwa ni kumpeleka mtoto (aliye na dalili zilizotajwa) kwenye kituo cha afya kutibiwa na kushauriana namna ya kuishi na ugonjwa humo.
Muhimu zaidi ni kuepuka kupata ugonjwa huu. Ikiwa una selimundu au vinasaba vyake, basi amua usizae na mtu mwenye selimundu au vinasaba vyake ili msizae mtoto mwenye selimundu au vinasaba vyake. Watu wanaotoka kwenye familia zenye vinasaba hivi ni vizuri kupima damu ili kujua kama una vinasaba. Ukijua una vinasaba, ni vyema kutafuta mwenzi asiye navyo.
Maelezo haya ya kitaalamu kupitia TANCDA, yanapaswa yalete tafakuri miongoni mwa jamii juu ya suala zima la watu wanaotarajia kuaona kupima damu kabla ya kuingia maisha ya ndoa. Hili ni suala ambalo halisisitizwi wala kuwekwa wazi kwani watu wengi huingia maisha ya ndoa bila kufahamiana hali ya afya.
Kwa vyovyote vile, watu wanapoingia maisha ya ndoa, shauku ya wengi huwa ni kupata watoto tena wenye afya. Hivyo jamii inapaswa kuelimishwa juu ya umuhimu wa wenza kupima damu kabla ya uamuzi wa kuzaa. Watakaokutwa wana vinasaba vya selimundu, waelezwe wazi kuwa wana uwezekano mkubwa wa kuzaa watoto wenye ugonjwa wa selimundu na wao wafanye uchaguzi kulingana na utashi wao.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages