Suala
la katazo la kuingiza filamu za nje nchini Tanzania limepokelewa kwa hisia
tofauti na watu wengi mimi ni mmoja wao ila kwangu nina mawazo tofauti na wengi.
Kama nilivyoanza kwa kusema hapo kwamba huwezi kuwa shujaa kwa
kumdidimiza shujaa mwingine, kwanza nisisitize hatuwezi kuboresha soko letu la
filamu kwa kufungia au kudidimiza soko la filamu toka kwingine ambalo
limeshakuwa kubwa na limeendelea kuboreshwa kwa muda mrefu kwa kutumia
ushirikiano wa sekta mbalimbali za nchi husika.
Ukiangalia filamu za kimarekani ambazo naamini ndizo zinazozungumziwa
hapa, kuna aina nyingi za filamu, zenye kulenga umri, jinsia, historia za kweli
au uwongo, matukio ya kweli, tamthilia, documentaries na mengine mengi na pale
unapoenda kununua kwa njia ya mtandao filamu husika huwa iko kwenye category
hizo hapo juu – kuhusu kufungia filamu za nje lile tamko halijasema ni za aina
gani kulingana na category nilizotaja hapo juu.
Mfano ukizuia documentaries za vitu kama historia, afya,
maonyesho ya sanaa muziki au silaha kila mtu atakushangaa maana mambo hayo ni
muhimu sana kwa watu kujifunza na kupata mengine yaliyowahi kutokea duniani,
yanayokuja na tuliyonayo sasa hivi na maisha kwa ujumla.
Mimi
huwa naangalia documentary 10 mpaka 20 kila mwezi zenye mafunzo mbalimbali na
baadhi nimeshiriki kuchangia script zake kwenye vipengele vinavyohusu sayansi
na tekinolojia.
Filamu nyingi za marekani zilizoanza kutoka mwaka 2010 mpaka
2017 utaona wakati zinaisha zina nembo iliyoandikwa State of Georgia imekuwa
hivyo kwasababu jimbo hilo lilihitaji kujitangaza fursa zake na mengine
yaliyopo na ikaonekana moja ya mbinu ni kuwekeza kwenye filamu kwa kukaribisha
wacheza filamu kurekodi movie kwenye vivutio vya maeneo mbalimbali ya jimbo
hilo na sasa hivi mapato yake yameongezeka zaidi ya mara 40 kutokana na mkakati
huu.
Ukitazama filamu za Uingereza utaona mara nyingine wanaonyesha
mto themes pamoja na daraja la London na vivutio vingine mbalimbali ambapo
watazamaji wa filamu hizo hutaka kwenda kutembelea kujionea masuala mbalimbali.
Kwa Tanzania tuna mbuga za wanyama Zaidi ya 5, milima mirefu,
miundombinu kama daraja la, kilombelo, mkapa na kigamboni; magorofa pacha pale
dar es salaam, Bagamoyo, Zanzibar, Ziwa Tanganyika, Nyasa, Victoria, Mabasi ya
Mwendo kasi, Visima vya gesi, Mashamba ya chai, Tumbaku, Kahawa, Viazi na
maeneo mengine mengi – maeneo haya yote yanaweza kutumika katika kuvutia
wacheza filamu wa nje au wa ndani kutengeneza filamu zao zenye ubora kwa
gharama nafuu au bila gharama kabisa lakini pesa zitarudi kwa kuuza filamu au
watu watakaopenda kutembelea maeneo hayo kwa nia ya kutalii au kuendeleza kwa
kufanya uwekezaji wa nguvu.
Ni suala la kuandaa kongamano kubwa la filamu au Sanaa kisha
kualika wadau mbalimbali wa sekta hiyo toka sehemu mbalimbali duniani ambao
watatembezwa katika vivutio vyote hivyo na kupewa offer ya gharama nafuu au
bure kabisa kutengeneza filamu za aina mbalimbali kisha kazi ianze mara moja.
Pia tuandae scholarship zitakazogharamiwa na serikali ya
Tanzania zenye lengo la kufanya tafiti mbalimbali zinazohusu Sanaa haswa filamu
katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ambapo tutaalika wanafunzi toka sehemu
mbalimbali za dunia kufanyia kazi lakini kwa lengo la kutangaza, kuvutia na
kutangaza fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta hii.
Vikundi vyote vya Sanaa za maigizo vinatakiwa kupewa ruzuku maalumu
kwa ajili ya kununua vifaa, kujiendeleza kimasomo na kimkakati, mikoa yote
lazima iwe na orodha ya wasanii wake na aina ya Sanaa wanazofanya napengine
maeneo wanayofanyia kazi zao ili kuweza kufuatiliwa na kusaidiwa kimkakati pale
itakapohitajika.
Katika kusemea masuala ya filamu na Sanaa kwa ujumla kuna Baraza
la Sanaa, COSOTA, na vyama vingine hawa wote wapewe fursa kuongea na kujadili
suala hili maana ni taasisi za kitaifa zinazotambulika sio za mkoa au wilaya.
Mwisho tukumbuke serikali yetu imeruhusu biashara huria kwahiyo
lazima tukubali kushindana kama wengine ili tushinde lazima tuboreshe kazi zetu
lazima kuthamini wazalishaji wetu lakini tuboreshe elimu na maeneo mengine
mengi ya kimkakati ili kuweza kupata kazi za uhakika.
Kuzuia au kufungua filamu za nje ni kujitenga na soko la
kimataifa je sisi tutauza wapi kazi zetu kama tunafungia zao? Ziendelee kuja
lakini kwa taratibu bila kuvunja haki miliki za watengenezaji husika.
No comments:
Post a Comment