Ikiwa ni siku moja toka biashara ya
filamu ‘feki’ za nje zipigwe marufuku mpaka pale wafanyabiashara wa filamu
hizo watakapokamilisha taratibu za ulipaji wa kodi, mengi yameendelea kuibuka,
ikiwa ni pamoja na wasanii ambao walihusika kwenye kampeni hiyo kuambiwa
wanatumika kisiasa.
Wasanii hao wakiongozwa na JB,
Jumatano hii waliungana na ofisi ya Mkoa wa Dar es salaam kufanya operesheni
hiyo ndani ya soko la Kariakoo kwa madai filamu hizo zinawanyonya wasanii wa
filamu wa ndani kwa kuwa zinauzwa bila kulipiwa kodi wakati wao filamu zao
zinalipiwa kodi.
JB amedai amesikitishwa kuona baadhi
ya watu wanalihusisha tukio hilo na siasa.
“Ndugu zangu kuna jambo naomba niongee na nyinyi, hivi mnajua tunayoyalilia
ni maisha yetu, kwanini kila kitu mnahusisha na siasa? Hivi ni haki mimi
nitozwe 30% ya pato langu mwingine asitozwe?,” aliandika JB Instagram.
“Kwenye shida mimi sitajali nani ananisaidia ilimradi anagusa
maslahi yangu, ugali wangu, ninakiri sinema zetu zina mapungufu mengi lakini
hiyo siyo sababu za kuacha kudai haki zetu.
Ni kama mgonjwa akiumwa leo
anapelekwa kwa mganga kesho anapelekwa kuombewa anatetea roho yake. Nawaomba
sana hatukatai mkitusema kuwa movie zetu zina matatizo lakini ngoja tumalize
hili, tusichanganye, na pia hakuna aliyesema zifungiwe hapana zifuate utaratibu
kama sisi tunavyo fata. Hizohizo movie zetu mbovu ndio zinatuwezesha kuishi,” aliongeza.
“Lakini pia lazima mfahamu biashara hii ni kubwa kuliko
mnavyodhania, movie 2 zinanitosha kuishi kwa mwaka mzima, ushawaza ni kiasi
gani mimi pamoja na kushiriki mapambano haya ni kama nimemaliza muda wangu
kwenye kazi hii nimebakiza movie 1 tu.
Je udhani mwanao au ndugu yako naye
anaweza kuingia huku? Tukiiponda tasnia huniharibii mimi tu, unaharibu maisha
ya watu wengi wajao ambao watafanya vizuri zaidi yetu,” alifafanua zaidi.
Sakata hili limewagawa wasanii wa
filamu nchini mara mbili. Wapo ambao wanaamini njia hiyo itasaidia kukuza
tasnia ya filamu huku wengine wakipinga njia hiyo kwa madai kua siyo sahihi
kwani filamu za nje zilikuwa nchini toka zamani.
No comments:
Post a Comment