Wanafunzi kadha wa shule moja
eneo la Sichuan, China wamepata ngazi mpya kuwasaidia kupanda na kushuka urefu
wa mita 800 kufika na kuondoka shuleni.
Kijiji cha Atuler kimepewa jina
la utani "kijiji cha mwamba". Kijiji hiki hupatikana mita 800 juu
kwenye nyika eneo la Sichuan, China. Wanaoishi hapa ni watu wa jamii ya Yi,
ambao pia hupatikana Vietnam na Thailand.
Hadi kufikia sasa, kulikuwa na
ngazi 17 za mbao ambayo ilikuwa njia pekee ya wakazi wa kijiji hiki kutoka nje
ya kijiji chao. Kupanda ngazi hizi lilikuwa jambo hatari na watu zaidi ya saba
walifariki wakizikwea, wakazi wanasema.
Watoto karibu 20 kutoka kijiji
cha Atuler husomea shule ya bweni, na ndipo waweze kufika hutakiwa kushuka kwa
kutumia ngazi hiyo. Wakati wa likizo, shule zinapofungwa, hutakiwa kupanda
ngazi tena kurejea kijijini.
Sasa, ngazi ya chuma imejengwa
kurahisisha safari yao. Lakini bado ni shughuli hatari, ingawa muda wanaotumia
kupanda na kushuka umepungua.
Watu wa jamii ya Yi wanaoishi
Atuler wamekuwa wakikwea mwamba huo kwa miaka na miaka na wana hata kanuni za
kupanda. Wakati wa kupanda, wanaume wanawajibika kuwabeba na kuwatunza watoto.
Watoto wa chini ya miaka 16 hawaruhusiwi kupanda au kushuka kwenye ngazi hiyo
wakiwa peke yao.
Ngazi hiyo ya chuma ilijengwa
baada ya habari za kijiji hicho kugonga vichwa vya habari kimataifa.
Ingawa wengi wanasifu ujenzi wa
ngazi hiyo, wapo watu wanaoshangaa ni kwa nini wanakijiji hao hawawezi kuhamia
eneo linalofikiwa kwa urahisi.
Lakini wakazi waliambia
wanahabari China kwamba hawataki kuacha nyumba zao, hasa kuhamia mijini ambapo
maisha wanaamini ni magumu sana.
No comments:
Post a Comment