Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan (kulia) Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete pamoja na viongozi
wengine wakiangalia kwa vitendo majaribio ya kiyasansi kutoka kwa wanafunzi wa
kidato cha sita wa shule ya sekondari ya WAMA NAKAYAMA kwenye sherehe za
mahafali yao ambapo wanafunzi 45 wamehitimu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu
Hassan amewahimiza wanafunzi kote nchini kupenda kusoma masomo ya Sayansi hasa
watoto wa kike ili Taifa liweze kujitosheleza kwa wataalamu wa fani mbalimbali
nchini hasa wakati huu ambao Taifa linaelekea kwenye uchumi wa Viwanda.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu
Hassan ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwenye mahafali ya Pili ya
wanafunzi wa Kidato cha Sita wa shule ya sekondari ya WAMA- NAKANYAMA Jijini
Dar es Salaam, mahafali ambayo imehudhuriwa na wake wa Marais Wastaafu.
Makamu wa Rais amesema haitapendeza hata kidogo ajira nyingi nchini
kuchukuliwa na wataalamu mbalimbali mataifa ya nje hasa kipindi hiki wakati
Serikali inahimiza ujenzi wa viwanda hivyo amesisitiza wanafunzi wajikite
kwenye kusoma masomo ya sayansi ili taifa liweze kujitosheleza kwa ajili ya
manufaa ya maendeleo ya taifa. Amesema katika kuhakikisha taifa lipata
wanasayansi wengi, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa maabara na
kununua vifaa vya maabara ili kuhamasisha wanafunzi wengi zaidi kupenda kusoma masomo
ya sayansi kote nchini.
Makamu wa Rais pia amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Tano
inakusudia kuimarisha ufundishaji wa masomo ya Teknolojia ya habari na
Mawasiliano –TEHAMA- katika shule za Sekondari na kujenga maabara za kompyuta
nia ikiwa ni kuongeza wataalamu wa fani hiyo nchini. Kuhusu mila na desturi
kandamizi kwa wanawake na wasichana zilizopo kwenye baadhi ya jamii nchini,
Makamu wa Rais ameitaka jamii kukomesha mila hizo na iwashirikishe wanawake
katika mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi kwani watakuwa ni chachu ya maendeleo
katika jamii husika.
“Wote tunajua wanawake ni chachu na kiungo muhimu katika maendeleo ya
jamii, Taifa na Dunia kwa ujumla hivyo ni wajibu wa jamii kushirikisha wanawake
katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo kote nchini” amesisitiza
Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais pia ameipongeza Taasisi ya Wanawake na Maendeleo – WAMA-
kwa kujenga shule Mbili za Sekondari na kusomesha watoto wanaotoka kwenye
familia maskini na yatima na kusema huo ni mfano wa kuingwa na wadau wengine wa
maendeleo katika kusaidia kundi hilo ili watoto wanaotoka kwenye familia
maskini nao waweze kuapata elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya baadae.
Kuhusu changamoto zinazoikabili shule ya WAMA – NAKAYAMA, Makamu wa Rais
ameahidi kushughulikia changamoto hizo ikiwemo uhaba wa maji, ubovu wa barabara
kuelekea kwenye shule hiyo na tatizo la uhaba wa mabweni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WAMA na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya
Nne Mama SALMA KIKWETE amesema aliamua kuanzisha taasisi hiyo ambayo inamiliki
shule Mbili mpaka sasa ili kusaidia watoto wa maskini na yatima kupata elimu
bure ambapo mpaka sasa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaliohitimu katika shule
hizo ambao wamejiunga na masomo ya elimu ya juu. Mama Salma Kikwete ameshukuru
ushirikiano mkubwa anaopata kutoka Serikalini unaolenga kuhakikisha shule
zinazoendeshwa na taaisisi hiyo ikiwemo ya Wama – Nakayama zinafanya vizuri.
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa WAMA Mama
Salma Kikwete(kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa WAMA Bi.Zakhia Meghji wakiimba
wimbo maalumu wa shule ya Sekondari ya WAMA NAKAYAMA wakati wa mahafali ya pili
ya kidato cha sita ambapo wanafunzi 45 wamehitimu.
Baadhi ya Wanafunzi
waliohitimu kidato cha sita katika shule ya sekondari WAMA NAKAYAMA.
Theresia Sanu (kulia)akisoma
hotuba ya wahitimu kwa Mgeni Rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa mahafali ya pili ya kidato cha sita
ya shule ya sekondari ya WAMA NAKAYAMA.
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye mahafali ya
pili ya kidato cha sita ya shule ya Sekondari ya WAMA NAKAYAMA ,ambapo aliwaasa
wanafunzi hao 45 kusoma zaidi ili waje kulisaidia Taifa lao.
Mwenyekiti wa WAMA Mama
Salama Kikwete akihutubia katika mahafali ya kidato cha sita ya shule ya WAMA
NAKAYAMA ambapo aliwataka wanafunzi hao kusoma na kufika juu zaidi.
No comments:
Post a Comment