Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere ulikuja hapa duniani Aprili 13, 1922 kupitia kwa Mpendwa Marehemu Bibi
Mgaya wa Buritho kama zawadi kwa nchi ya Tanzania.
Mwalimu tunamshukuru
Mungu kwa kutupa wewe ambaye umeitendea mambo makubwa Tanzania, Afrika na Dunia
kwa ujumla.
Mwalimu wakati nakumbuka
kuzaliwa kwako nimepata fursa ya kuangalia kazi ulizozifanya mara baada ya
kuacha madaraka ya Urais na kujikita katika kazi kuu tano; Mosi pamoja na
kubaki na kofia moja ya Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya kuimarisha
Chama na alianza maandalizi ya kukabidhi Uenyekiti huo kwa Rais aliyepokea
madaraka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa Rais Mstaafu wa
Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Pili, mwaka 1986 baadhi ya Viongozi wa nchi za Kusini mwa Dunia, walikuomba
kuanzisha Tume ya Uchambuzi wa maendeleo ya nchi za Kusini tangu miaka 30
iliyopita na kuweza kuona hatua za maendeleo na changamoto zilizopo katika
mataifa hayo na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuboresha ustawi wa wananchi.
Mwalimu Nyerere alikubali
jukumu hilo, ndipo alianza kutembelea nchi 19 katika Bara la Asia na Marekani
ya Kusini kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa majukumu hayo mapya. Safari ya
kutafuta maoni hayo ilikuwa ni pamoja na kupata uthibitisho wa kuwaelewesha
wananchi na nchi hizo kuhusu majukumu ya Tume na aina ya maoni yanayokusanywa.
Kazi hiyo aliifanya kwa
miaka mitatu na kutoa ripoti kuwa nchi za Kusini zifanye maendeleo yao yenyewe
yalenge maslahi ya wananchi walio wengi kwa kielelezo kuwa ili nchi za Afrika
ziweze kupiga hatua za maendeleo ni vyema ziwe na mshikamano kama zinahitaji
kushindana na nchi za Kaskazini.
“Nchi za Kusini
zishirikiane kibiashara, kwa kuwa nchi za Kusini zina mazoea ya kufanya
biashara na nchi za Kaskazini lakini hakuna utaratibu mzuri wa nchi za Kusini
kufanya biashara wenyewe kwa wenyewe, au hata katika uwekezaji rasilimali”
alisema Mwalimu Nyerere.
Aidha, Mwalimu Nyerere
alisema Wataalam wengi wako Kusini lakini nchi za Kusini zinatafuta wataalam
kutoka Kaskazini, hivyo ni wajibu wa nchi za Kusini kujenga na kuimarisha
ushirikiano wa pamoja baina yao.
Tatu, Mwalimu alianzisha kituo cha muda cha Nchi za Kusini pale Geneva
ambapo Mwalimu na Viongozi wengine walifanya kazi kwa muda wa miaka miwili,
jukumu lao likawa kuelezea shughuli za maamuzi na mapendekezo ya Tume.
Nne, kuanzisha Ofisi ya kudumu ya Nchi za Kusini pale Geneva kwa ajili ya
Mataifa hayo kutoa hoja kupitia vuguvugu la nchi za kundi la 77 ambazo hazikuwa
na chombo cha kuwasaidia kupaza sauti zao.
Mwalimu akapokea jukumu
hilo na kuanzisha Ofisi ya kudumu ambayo ilikuwa chombo cha Serikali badala ya
chombo cha kiraia na kuhusisha nchi 49 ambazo ziliweka sahihi, pamoja na nchi
kubwa ulimwenguni ikiwemo India, Brazil na Afrika ya kusini.
Tano, alikuja na wazo la
kuanzisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere, hatua iliyotokana na harakati za kazi
yake ya kuunganisha nchi za kusini, ambapo alitaka taasisi hiyo kufanya kazi
zake katika ukanda wote wa nchi za Bara la Afrika.
Miongoni mwa kazi hizo ni
pamoja na kuangalia maendeleo ya watu, kupitia dhana ya umoja na ushirikiano
miongoni mwao.
Nakumbuka hotuba ya
Mwalimu Nyerere aliitoa mwezi Februari mwaka 1960, akiwa Rais wa chama cha
Tanganyika African National Union (TANU) , alikaribishwa nchini Marekani katika
Kongamano la Afrika katika Chuo cha Wellesley Massachusetts kuongelea kuhusu
“Nafasi ya Afrika Duniani”.
Katika hotuba hiyo,
Mwalimu alizungumzia hatua mbalimbali za ukombozi wa Bara la Afrika, mchango wa
Waafrika katika Mataifa ya Ulaya na Marekani. Mwalimu alilisemea Bara la Afrika
Kama Bara la matumaini kwa ubaguzi wa rangi.
Mwalimu alisisistiza kwa
kusema “Muda utafika ambapo Marekani na Ulaya Magharibi watajisikia vibaya
jinsi walivyoitumia Afrika” huku akitolea mifano ya mateso na manyanyaso
waliyoyapata Waafrika ikiwemo vita vya Mau Mau nchini Kenya, vifo vya watu wa kabila
la Waherero nchini Namibia, vita vya Majimaji nchini Tanzania.
Hotuba hiyo ilikuwa ya
kwanza kwa Mwalimu Nyerere kuchapishwa kimataifa, hakika imeonyesha kwa dhati,
Mwalimu hata kabla ya Uhuru alitambua nafasi ya umoja katika kupigania uhuru wa
Bara la Afrika.
Aidha, ndoto hii ya umoja
alisafiri nayo katika kujenga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nafasi ya
Uenyekiti Jumuiya wa Nchi zilizo mstari wa mbele katika Ukombozi Kusini mwa
Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) na nyingine nyingi.
Taasisi ya Mwalimu
Nyerere dhumuni lake kuu ni kuendeleza Amani, Umoja na Utulivu wa Maendeleo ya
pamoja Barani Afrika. Mwalimu alikuwa muanzilishi na Mweneyekiti wa kwanza wa
Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Septemba 14, 1996
alikaribishwa Kilimanjaro hoteli kuhutubia na kuzindua Taasisi ya Mwalimu
Nyerere. Umuhimu wa Umoja, umuhimu wa ukubwa wa soko, Amani baina ya nchi ndani
na nje ya nchi na Maendeleo katika Afrika.
Alipata fursa ya kukutana
na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwaeleza juu ya Taasisi hiyo
na madhumuni yake. Katika kipindi hiki Mwalimu alikuwa msuluhishi wa mgogora wa
Burundi.
No comments:
Post a Comment