Dar es Salaam, TANZANIA. Taasisi na Asasi Zisizokuwa za
Kiserikali za Tanzania (NGOs) taasisi za serikali zinazoshughulikia uwajibikaji
na wadau wengine kadhaa walikutana hivi leo ili kufanya tathmini ya hatua
zilizopigwa na mafunzo yaliyopatikana wakati wa uhai wa mradi wa Pamoja
Twajenga unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la
Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Toka mwaka 2013, watendaji wa mradi wa Pamoja Twajenga wamekuwa wakifanya kazi bega kwa bega
na asasi za kiraia na taasisi za serikali ya Tanzania zinazoshughulikia masuala
ya uwajibikaji ili kuimarisha mahusiano kati ya asasi za kiraia na serikali.
Mradi huu ulitoa mafunzo na msaada kwa jumla ya asasi zisizo za Kiserikali 16
na taasisi tatu za serikali zinazojihusisha na uwajibikaji katika mikoa ya
Mtwara, Iringa, Dodoma, Morogoro na Zanzibar kwa lengo la kukuza uwazi na
uwajibikaji wa serikali kwa raia wa Tanzania.
Kutokana na msaada huu, hivi sasa asasi za kiraia na taasisi za
uwajibikaji zilizoshiriki zina uwezo zaidi wa kushiriki katika mijadala kuhusu
masuala mahsusi yanayozigusa jamii (issue-based dialogue).
Raia katika mikoa lengwa ya mradi – ikiwa ni
ni pamoja na vijana, wanawake na makundi mengine ya watu wanaowekwa pembezoni
wana uwezo zaidi wa kujadiliana na serikali zao kuhusu kero zao, jambo ambalo
limeongeza uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa rasilimali za umma na
katika ufanyaji maamuzi. Asasi za kiraia zilizosaidiwa na mradi wa Pamoja Twajenga zinafanya kazi katika masuala yanayohusiana
moja kwa moja na mahitaji ya msingi ya raia ikiwa ni pamoja na huduma za afya,
elimu, usalama wa chakula na usimamizi wa rasilimali.
Mathalan, wanakijiji katika kijiji cha Kibaigwa, mkoani Dodoma walikuwa
wakilazimika kwenda umbali wa kilomita 45 ili kupata kituo cha afya chenye
huduma ya wodi ya wazazi. Asasi ya Kiraia iliyofadhiliwa na mradi huu itwayo
TACOSODE,iliwasaidia wanakijiji hao kujadiliana na uongozi wa kijiji chao
kuhusu haja ya kumalizia wodi mpya ya akinamama. Mjadala huo uliifanya kamati
ya kijiji kuwasilisha katika serikali ya wilaya ombi la fedha kwa ajili ya kazi
hiyo. Ujenzi wa wodi hiyo ulikamilika mwezi Oktoba 2015 na hivi sasa inahudumia
jamii.
Asasi nyingine
iliyosaidiwa na mradi wa Pamoja Twajenga ni Chama cha Wanasheria watetezi wa
Mazingira (LEAT) ambayo ilitoa mafunzo ya usimamizi wa maliasili na uwajibikaji
kwa jamii (social accountability) kwa kijiji cha Kiwere mkoani Iringa. Mafunzo
haya yaliwawezesha wanakijiji kuchukua hatua ya kutaifisha mbao ambazo zilikuwa
zimevunywa isivyo halali katika ardhi yao.
Kupitia misaada mbali mbali kwa asasi za Kiraia za Kitanzania na
taasisi za serikali za uwajibikaji mradi wa Pamoja Twajenga umesaidia
kuimarisha mfumo wa majadiliano na ushiriki ambapo asasi zinaweza kupata
matokeo makubwa na endelevu zikiwa kama asasi za ushawishi na utetezi katika
sekta zao mahsusi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa
leo, Naibu Mkurugenzi wa USAID nchini Tanzania David Thompson alisisitiza,
“mradi huu umejielekeza katika azma moja kuu iliyo rahisi kueleweka: kwamba
mstakabali wa Tanzania unategemea ushiriki huru na imara wa raia kutoka katika
nyanja zote za maisha. Nyote mliokusanyika hapa hivi leo, iwe mnawakilisha
asasi za kiraia au Serikali ya Tanzania mmekuwa na mchango mkubwa katika
kufikia azima hii. Asanteni kwa ubia wenu. Tanzania imechukua
hatua muhimu katika kuinua uwazi, kuimarisha utoaji huduma za jamii,
kuhakikisha kuwepo kwa nafasi ya kidemokrasia na kuwasaidia raia kuchagiza
mabadiliko.”
No comments:
Post a Comment