Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Baraza
la Habari Tanzania (MCT) uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
kubadilishana nao mawazo. Kulia ya Balozi Seif ni Katibu Mtendaji wa Baraza la
Habari Bwana Kajubi Mukajanga na Kushoto ya Balozi ni Mkuu wa Ofisi ya Baraza
la Habari Tanzania (MCT) upande wa Zanzibar Bibi Shifaa Hassan.
Mkuu wa Ofisi
ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) upande wa Zanzibar Bibi Shifaa Hassan
akifafanua jambo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
walipokutana nae kwa mazungumzo.
Katibu Mtendaji wa Baraza
la Habari Bwana Kajubi Mukajanga Kulia ya Balozi Seif akielezea mikakati ya
Baraza la Habari Tanzania inavyofanya kazi Zanzibar katika kuhakikisha Maadili
ya Habari yanazingatiwa na Wana Habari wote Nchini.
Katibu Mtendaji wa Baraza
la Habari Bwana Kajubi Mukajanga akimkabidhi Balozi Seif Vitabu mbali mbali
vilivyochapishwa na Baraza hilo kuhusu Tasnia ya Habari Tanzania.
Balozi Seif
akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa juu wa Baraza la Habari Tanzania
mara baada ya kubadilishana mawazo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kushoto
ya Balozi Seif ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Bwana Kajubi Mukajanga na
Muandishi wa Makala wa MCT Yussuf Mpinga. Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Ofisi ya
Baraza la Habari Tanzania (MCT) upande wa Zanzibar Bibi Shifaa
Hassan, Muhariri wa Machapisho wa MCT Khamis Mzee na Mkuu wa Kitengo cha
Rasilmali Watu cha MCT Bivi Ziada Kilobo.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inasubiri kuyapokea kwa ajili ya kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa
ya Rasimu ya Sera ya Habari Zanzibar katika kuona Sekta ya Habari Nchini
inakuwa imara.
Alisema
Taasisi zinazohusika na jukumu la kusimamia masuala hayo ni vyema zikahakikisha
kwamba zinaharakisha mapendekezo hayo ili ile dhana ya Uhuru wa kupata Habari
bila ya kuogopa inapatikana.
Balozi Seif
Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Baraza la
Habari Tanzania (MCT) ulioongozwa na Katibu Mtendaji wake Bwana Kajubi
Mukajanga aliokutana nao hapo Afisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kutoa kila aina ya msaada katika
kuona Sekta hiyo muhimu kwa jamii inawajibika ipasavyo katika kuwapasha Habari
Wananchi.
“Habari ni
Sekta muhimu inayotoa Taarifa na Elimu na kuwahusisha moja kwa moja Wananchi wa
kawaida wakiwemo wakulima Vijijini ”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar.
Balozi Seif
kupitia Uongozi wa Baraza hilo la Habari Tanzania aliwakumbusha Wana Habari
kuzingatia sheria na Maadili yao ya kazi katika kuandika Habari wanazozifanyia
Utafiti wa kina ili zisaidie Wananchi kupata Habari za ukweli.
Akizungumzia
changamoto ya Vitambulisho vya Kazi inayowakumba Wana Habari wanaotokea
Tanzania Bara na kupangiwa kufanya kazi Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliahidi kulifuatilia kwa kina suala hilo ambalo bado halijawa kero
kama yalivyo masuala mengine katika utendaji.
Alisema
Waandishi wa Habari wanaotokea Tanzania Bara wanapaswa kuandaliwa utaratibu
maalum wa kupata vibali vya kazi kwa vile wao hawahusiani na kuwa na
Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi katika kuomba kibali cha kufanya Kazi
Zanzibar.
Balozi Seif
alieleza kwamba mfumo unaotumika katika kuwapasha Habari Wananchi wa pande zote
za Muungano hauna mipaka licha ya kwamba Sekta ya Habari sio Taasisi iliyomo
ndani ya masuala ya Muungano.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT)
kwa umakini wake wa kusimamia Sekta ya Habari Nchini Tanzania.
Mapema Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Bwana Kajubi Kukajanga
alisema Kamati ya Maadili ya Bahara la Habari Tanzania imekuwa na utaratibu wa
kufanya ziara za kusikiliza malalamiko yanayotolewa na Wananchi wanaoandikwa
visivyostahiki katika Vyombo mbali mbali vya Habari.
Bwana Kajubi
alisema Wajumbe wa Kamati hiyo kupitia ziara hizo hupata fursa za kushauri,
kuelekeza pamoja na kuwaonya na wengine kuwachukuliwa hatua za kisheria Wana
Habari wanaofanya makosa katika kuandika Habari chafu dhidi ya wananchi mbali
mbali.
Alisema Viongozi
hao pia wanajaribu kusaidia Wana Habari wanaotoka Tanzania Bara kuondokana na
ukakasi wa kupata Vitambulisho vitakavyowapa fursa ya kufanyakazi kwa upana
zaidi bila ya vikwazo.
Naye Mkuu wa
Ofisi ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) upande wa Zanzibar Bibi
Shifaa Hassan alisema Mchakato wa Sera ya Habari Zanzibar umeanza tokea mwaka
2010 kwa mashirikiano baina ya Idara ya Habari Maelezo, Tume ya Utangazaji
Zanzibar pamoja na baadhi ya Viongozi wa Taasisi za Serikali.
Bibi Shifaa
alisema Zanzibar imekuwa tajiri katika masuala ya Historia ya Habari kutokana
na kuanza mapema kwa Sekta hiyo ndani ya Ukanda mzima wa Afrika ya Mashariki.
Alisema Ofisi
ya Baraza la Habari Tanzania upande wa Zanzibar ilianzishwa mwaka 2003 na
kuanza na Mpango Maalum wa harakati za kutoa mafunzo kwa Wana Habari wachanga
wa vyombo mbali mbali vya Habari wakiwemo pia wale waliomaliza masomo yao ya
sekondari walioamua kujiunga na Tasnia hiyo.
Bibi Shifaa
alieleza kwamba mpango huo ulikwenda sambamba na kutoa machapisho ya vitabu
mbali mbali, kufanya utafiti kuhusu shirika la Habari Zanzibar mambo yaliyoibua
kupatikana kwa Kitabu cha Historia ya masuala ya Habari Zanzibar
kilichozinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mwaka ulipita.
Viongozi wa
Baraza la Habari Tanzania tayari wapo Visiwani Zanzibar kuhudhuria maadhimisho
ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani inayofikia kilele chake ifikapo Tarehe 3 Mei
ya kila mwaka ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
No comments:
Post a Comment