Bw Peter Solomon Gichira anadaiwa kujaribu kujirusha kutoka
ghorofa ya sita katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) jijini Nairobi
baada ya ombi lake la kutaka kuwania urais kukataliwa Jumamosi jioni.
Mgombea mwenza wa Bw Gichira,
Kelly Watima, hata hivyo alisema mwenzake amekuwa akihangaishwa tangu
alipotangaza nia ya kutaka kuwania urais.
"Bw Gichira amekuwa akihangaishwa na maafisa wa IEBC na sasa
polisi wanamzuilia ndipo akose fursa ya kuwasilisha karatasi zake za uteusi
…mbona wanamuogopa…je, ni kwa sababu ni tishio kwao?" alisema, kwa mujibu
wa Daily Nation.
Bw Gichira ni miongoni mwa wanasiasa kumi waliokuwa wameeleza
nia ya kutaka kuwania urais lakini wakakosa kuidhinishwa na tume hiyo kwa
kukosa kutimiza amsharti mbalimbali.
Kuna wagombea kumi walioidhinishwa, ambao wamekuwa wakiwasilisha
karatasi zao Jumapili na leo Jumatatu.
Miongoni mwa waliofanikiwa kuwasilisha karatasi zao Jumapili ni
aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, mgombea huru Ekuru Aukot na Abdouba Dida
ambaye pia aliwania urais mwaka 2013.
Waliopangiwa kuwasilisha karatasi zao za uteuzi leo ni pamoja na
Rais Uhuru Kenyatta ambaye anawania kwa mara ya pili.
Mkuu wa polisi wa Nairobi Japheth Koome amesema Bw Gichira
atafunguliwa mashtaka ya kuzua fujo eneo la umma, kuharibu mali na kujaribu
kujitoa uhai.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, mkuu wa polisi wa kituo
cha Central Robinson Thuku alisema Bw Gichira alikuwa ameenda afisi za IEBC
kufuatilia ombi lake alipofahamishwa kwamba ombi lake lilikataliwa.
Ni hapo ambapo alianza kulalamika na akavunja dirisha na
kujaribu kuruka nje lakini akazuiwa na maafisa wawili ambao pia walimkamata.
Bw Thuku alisema mwanasiasa huyo atafikishwa mahakamani
Jumatatu.
Polisi walikataa kumwachilia dhamana na kusema wanamzuilia kwa
ajili ya usalama wake.
No comments:
Post a Comment