Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) Bw. Kailima Ramadhani akitoa elimu ya mpiga kura kupitia redio A FM ya
mkoani Dodoma leo Mei 9 mwaka huu huku akifuatiliwa kwa makini na watangazaji
wa redio hiyo.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) imetoa wito kwa wananchi walioko kwenye halmashauri mbalimbali nchini,
kuitumia vyema fursa ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia redio za kijamii
kwenye halmashauri zao ili kuondoa manung’uniko kwenye chaguzi.
Wito huo
umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Kailima Ramadhani wakati
akizungumzia mpango wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima ulioanza
kutekelezwa Mei 8 mwaka huu hii katika mikoa kumi nchini.
Alisema kupitia mpango
huo wananchi wanaosikiliza redio za kijamii kwenye halmashauri nchini, watapata
fursa ya kujifunza elimu ya mpiga kura na kuelewa masuala yote muhimu
yanayohusu mfumo mzima wa kupiga kura.
“Tumepanga mpango, Tume
itasambaa nchi nzima kuzungumzia elimu ya mpiga kura kwenye redio za kijamii
zilizoko kwenye halmashauri zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” alisema
Bw. Kailima.
Alisisitiza kwa kutoa
wito kwa wananchi walioko maeneo ambayo Tume itakwenda kutoa elimu ya mpiga
kura, wasikilize na kuuliza maswali ili waweze kuelewa.
“Hii ni fursa kwa
wananchi ambayo muda mrefu hawajawahi kuipata, hivyo nawaomba wafuatilie ili
waweze kuelimika zaidi ili yale manung’uniko ya kura yatakuwa yamekwisha na
tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi ya ile ambayo tumeifanya.” Alifafanua Bw.
Kailima.
Utekelezaji wa mpango huo
umegawanyika katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza limeanza kutoa elimu
hiyo elimu hiyo kwenye mikoa ya Kagera,Mwanza, Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya na
Dodoma.
Mikoa mingine
itakayojumuishwa kwenye kundi hilo ni Ruvuma, Mara, Pwani na Mtwara ambapo
elimu hiyo itatolewa kuanzia tarehe 8 Mei hadi tarehe 20 Mei mwaka 2017.
Kundi la pili
linatarajiwa kutoa elimu hiyo kuanzia tarehe 24 Mei hadi tarehe 7 Juni mwaka
huu katika mikoa ya Geita, Tanga, Singida, Shinyanga, Lindi, Arusha, Tabora,
Kigoma, Iringa, Manyara, Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe na Simiyu.
Bw. Kailima alisema kuwa
utoaji wa elimu hiyo utajikita kwenye mada kuu ya Elimu ya Mpiga Kura
iliyogawanywa kwenye vipindi vitano, itakaytoolewa kwenye redio hizo kulingana
mada husika na wananchi kuuliza maswali na kujibiwa na wawasilishaji wa mada
hizo kutoka Tume.
“Ni mada ambayo
imejumuisha masuala yote muhumu yatakayofanya mpiga kura yeyote au mdau yeyote
wa uchaguzi kuisoma au kuisikiliza na akaelewa mfumo mzima wa masuala ya kupiga
kura” alisema.
Mbali na kutoa elimu ya
mpiga kura kupitia vituo vya redio za kijamii katika halmashauri nchi nzima,
Tume pia inatoa elimu hiyo kwa njia ya magazeti na vyombo vingine vya habari na
mitandao ya kijamii, kushiriki kwenye mikutano na maonesho mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment