Ofisa Programu wa Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP), Alphonce Slima, akiongoza semina ya kujadili vipaumbele
katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 iliyofanyika makao makuu ya TGNP Mabibo
jijini Dar es Salaam jana.
Mdau Neofita Kunambi
akizungumza wakati akichangia mada kwenye semina hiyo.
Anna Sangai akichangia jambo
kwenye semina hiyo.
Sadick Juma mkazi wa Mbezi
Beach, akielezea changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika
Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili.
Janeth Mawinza akielezea
changamoto ya matibabu ya homa ya ini ambayo dawa zake hazipatikani nchini hadi
zitoke India.
Moses Benard akizungumzia
wajawazito kujinunulia vifaa vya kujifungulia na suala la dawati la ukatili wa
kijinsia kuwepo vituo vya polisi.
Mdau Dalia Kalungwana
akichangia jambo.
Washiriki wakiwa kwenye semina
hiyo.
Semina ikiendelea.
Wananchi wakifuatilia kwa
karibu semina hiyo.
Vijana wakifuatilia mada katika
semina hiyo.
WANANCHI wameiptia bajeti
ya mwaka 2017/ 2018 ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na
Watoto iliyotengwa na kuomba iongezwe kwa kuzingatia ukubwa wa wizara hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mtandao wa Kijinsia
Tanzania (TGNP) ya majadiliano ya kupitia bajeti hiyo ili kuona vipau mbele
vyake waliombwa iongezwe ili iweze kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye
wizara hiyo ambayo imelemewa kutokana na ukubwa wake.
Kwa mwaka wa fedha wa
2016/ 2017 wizara hiyo ilitengewa bajeti ya sh.bilioni 845 ikilinganishwa na
mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambayo tofauti yake sio kubwa.
Akizungumza katika semina
hiyo, Neofita Kunambi alisema katika wizara hiyo kunachangamoto kubwa bila ya
kuongezewa fedha katika bajeti yake hazitaweza kuisha.
"Bila ya kuongeza
bajeti katika wizara hii wajawazito wataendelea kujinunulia vifaa vya
kujifungulia tunaomba jambo liangaliwe kwa karibu" alisema Kunambi.
Anna Sangai alisema
huduma za afya zinapaswa kuboreshwa kuanzia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
na bila kuongezwa kwa bajeti katika wizara hiyo itakuwa ni ndoto.
Mkazi wa Mbezi Beach,
Sadick Juma alisema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, miundombinu na ukatili wa
kijinsia ni changamoto kubwa katika wizara hiyo.
Alisema licha ya kuwepo
duka la Bohari ya Dawa (MSD) katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili
(MNH), upatikanaji wa dawa umekuwa mgumu hivyo kuifanya Muhimbili kuwa na
majengo mazuri bila ya kuwa na dawa.
"Ukitaka kuona
changamoto hata ukiwa ni mwanachama wa mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF)
ugua au uwe na mgonjwa ambaye ni mwanachama uende katika hospitali hiyo kwanza
kupokelewa tu pale mapokezi ni balaa na ukifika muda wa kutakiwa kupata dawa
utaambulia panado na kuambiwa dawa hazipo" alisema Juma.
Juma aliongeza kuwa
huduma ya bure kwa watu wenye msamaha hiyo ni ndoto kwani wagonjwa hao
hawasikilizwi kabisa jambo ambalo ni hatari.
Alisema serikali imekuwa
ikijipodoa kuwa inaboresha huduma za afya lakini hali halisi haipo hivyo
akitolea mfano kwa nchi nzima maduka ya dawa ya MSD yapo nane tu je upatikanaji
wa dawa na vifaa tiba utafikia katika kiwango cha kukidhi mahitaji alihoji
Juma.
Janeth Mawinza alisema
bajeti hiyo iangalie zaidi jinsi ya kutibu magonjwa kama ya homa ya ini ambayo
matibabu yake kwa hapa nchini hayapatikani mpaka dawa itoke nchini India.
Moses Benard alisema
ikiwa mjamzito aliopo mjini anatakiwa kujinunulia vifaa vya kujifungulia hali
ikoje kwa yule ambaye yupo kijijjini ambaye anachangamoto ya kutokuwa na fedha
na kukimbiwa na mwenza wake hivyo akaomba Waziri wa wizara hiyo kutoa tamko
rasmi la kuwataka wajawazito kutonunua vifaa hivyo wanapokwenda hospitali
kujifungua.
Wadau wengine waliongelea
jijini Dar es Salaam maeneo mengine kama Kipunguni wilayani Ilala kukosa kuwa
na zahanati au hospitali hivyo kulazimika kwenda wilaya ya Kisarawe kupata
matibabu jambo ambali linashangaza hivyo wakaomba bajeti ya wizara hiyo
iongezwe ili kufanikisha upatikanaji wa zahanati au hospitali katika maeneo
yao.
No comments:
Post a Comment