Meneja wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Gabriel
Mwangosi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu semina juu
ya Kodi, Utaratibu na Sheria kwa wafanyabiashara kutoka China iliyoandaliwa kwa
ushirikiano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC) pamoja na Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd na kufanyika leo Jijini Dar
es Salaam katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.
Mrakibu wa uhamiaji
na Afisa Vibali vya Ukazi, Eliud Ikomba akitoa semina kwa wafanyabiashara
kutoka China (hawapo pichani) juu ya sheria za uhamiaji katika semina
iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd na kufanyika
leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.
Baadhi ya wafanyabiashara kutoka China wanaofanya
biashara zao nchini wakisikiliza mafunzo mbalimbali juu ya Kodi, Utaratibu na
Sheria katika semina iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na Kampuni ya Jiteng
Consultancy Ltd na kufanyika leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa
Makumbusho ya Taifa.
Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imetoa somo la masuala ya kodi kwa wafanyabiashara kutoka China
wanaoishi nchini kwa lengo la kuwaongezea uelewa juu ya sheria na taratibu za
ulipaji kodi katika semina kuhusu mafunzo hayo leo Jijini Dar es Salaam.
Akiwasilisha mada wakati
wa mafunzo hayo, Meneja wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA,
Gabriel Mwangosi amesema kuwa Tanzania ya sasa ina fursa nyingi za uwekezaji
hivyo wafanyabiashara hao watakapokuja kuwekeza lazima wafahamu kanuni na
taratibu za ulipaji kodi nchini ili waweze kuendana na sheria zilizopangwa na
nchini.
“Semina
hii mahususi imeandaliwa kwa ajili ya wafanyabiashara wa kichina wanaoishi
nchini kupata mafunzo ya kodi zikiwemo za zuio, majengo pamoja na ushuru na
forodha ambazo ni lazima wazifahamu kwa manufaa ya Taifa letu na wao pia,”alisema Mwangosi.
Mwangosi ameongeza kuwa
hii ni mara ya 6 kufanyika kwa semina hizo kwa wafanyabiashara hao ambapo tangu
zianze kufanyika zimewasaidia kutokwenda kinyume na taratibu zilizowekwa nchini.
Kwa upande wake Kaimu
Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC), Dotto Stanley amesema kuelimisha umma hasa kwa wageni kutoka nje ya nchi
ni jambo la msingi litakalowarahisishia kufahamu sheria za nchi ambapo kwa
namna nyingine itachochea uwekezaji.
“Kwa
kawaida wafanyabiashara wakubwa huwa wanahitaji kufahamu sheria na taratibu za
nchi husika kabla hawajaamua kuwekeza mahali hivyo mafunzo hayo yatachochea
uwekezaji nchini kwa sababu watakuwa na uelewa wa mchakato mzima juu ya sheria
za uwekezaji na kodi.”alisema
Stanley.
Naye Mkurugenzi wa
Uendeshaji kutoka Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd, Anne Werema Maneno amesema
kuwa changamoto kubwa inayowapata wafanyabiashara wa kichina ni kukosa uelewa
juu ya jinsi ya kuwekeza nchini hasa katika suala la ulipaji kodi.
“Changamoto
hiyo inawapelekea wafanyabiashara kukosa muelekeo wa biashara waliyopanga
kufanya kwani wengi wao wakifika Tanzania hubadilisha biashara baada ya
kufahamishwa sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu biashara hivyo semina hiyo
itawapa uelewa utakaowawezesha kuchagua biashara watakayoweza kuifanya
kulingana na mtaji wa mfanyabiashara husika,”alisema
Bi. Anne.
Aidha, katika semina hiyo
ya siku moja imeambatana na fursa ya kupata mafunzo kutoka kwa taasisi zingine
zinazofanya kazi moja kwa moja katika shughuli ya uwekezaji ambazo ni pamoja na
TRA, TIC, Idara ya Uhamiaji, Idara ya Kazi pamoja na Taasisi za Kibenki.
Mafunzo hayo juu ya Kodi,
Utaratibu na Sheria kwa wafanyabiashara hao yameandaliwa kwa ushirikiano wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na
Kampuni ya Jiteng Consultancy Ltd na kufanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya
Taifa ikiwa ni utaratibu wa kawaida wakukutana na wadau mbalimbali wa Kodi.
No comments:
Post a Comment