Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kati, Ikwiriri, Athuman Mtoteka
anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.
Mwenyekiti huyo ambaye anawakilisha chama cha Wananchi CUF, anadaiwa
kutekwa jana kati ya saa moja na mbili usiku.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,
Onesmo Lyanga amesema watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake kwa miguu
kisha kumchukua na kwenda naye kusikojulikana.
Amesema taarifa za tukio hilo zilitolewa katika kituo cha Polisi
Ikwiriri leo Alhamisi asubuhi na mkewe.
Lyanga ameeleza kuwa baada ya kutolewa kwa taarifa hizo kituoni hapo,
Polisi tayari wamefungua jalada la uchunguzi dhidi ya tukio hilo.
"Tumepokea taarifa hizo toka kwa mkewe akielezea mumewe
kuchukuliwa na watu wasiojulikana na kuondokanae kusikojulikana" amesema
Lyanga.
Kadhalika taarifa toka kwa majirani wa mwenyekiti huyo zinaeleza kuwa
waliwaona watu watano waliofika nyumbani hapo wakitembea kwa miguu kisha
kumkamata na kuondoka naye.
Katika tukio jingine, maiti ya mtu mmoja ambaye hajatambulika jina lake
imekutwa ikielea ndani ya Mto Rufiji, Kitongoji cha Ngwalo kilichopo katika
Kijiji cha Mtunda A, wilayani Kibiti.
Kamanda Lyanga amesema uchunguzi wa daktari juu ya maiti hiyo
ulionyesha marehemu alikuwa na jeraha moja kichwani lililotokana na kupigwa
risasi.
Lyanga amesema marehemu alikuwa amefungwa kamba katika mikono yake yote
na maiti hiyo ilikuwa imeanza kuharibika kutokana na kukaa majini kwa muda
mrefu.
Amesema kutokana na maiti hiyo kuanza kuharibika waliuruhusu uongozi wa
kijiji hicho kuizika jana Jumatano.
Amesema baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliiona maiti hiyo ikielea
majini kwenye mikondo ya maji ya Mto Rufiji kisha kutoa taarifa kwa uongozi wa
kijiji hicho nao waliotoa taarifa Polisi.
Kutokana na matukio hayo, Jeshi la Polisi mkoani Pwani kupitia kwa
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Onesmo Lyanga limetoa wito kwa wananchi waishio
katika wilaya za Kibiti na Rufiji kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vya
mauaji yanayozidi kutokea katika wilaya hizi mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment