MSHAMBULIAJI mpya wa Klabu Bingwa ya
Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Wazir Junior, amewatoa wasiwasi mashabiki wa
timu hiyo akiwaambia kuwa hatowaangusha.
Junior aliyesaini mkataba wa miaka
miwili kujiunga na timu hiyo jana, ameyasema hayo wakati akitambulishwa leo
asubuhi na Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, aliyekuwa sambamba na Meneja wa
timu, Phillip Alando na Meneja wa mchezaji huyo, Abdallah Bawazir.
Mshambuliaji huyo amesema kuwa
anafurahishwa kujiunga na Azam FC huku akidai zilikuwa ni ndoto zake za muda
mrefu kutua kwa mabingwa hao.
“Kwanza namshukuru mwenyezi Mungu kwa
kujiunga na Azam FC, pili naishukuru timu yangu ya Toto African niliyocheza
misimu miwili, nashukuru ushirikiano wa wachezaji wenzangu pamoja na viongozi
na mashabiki, kingine nimefurahi kujiunga na Azam FC,” alisema.
Alisema kuwa anaamini ya timu hiyo
ndio mahali pake sahihi kwa kuendeleza kipaji chake huku akidai kuwa
itamwezesha kufika mbali kwa kutimiza malengo yake ya kufika mbali yaani
kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
“Kwa hiyo nahitaji tu ushirikiano kwa
mashabiki na wachezaji wenzangu, mashabiki wasiwe na wasiwasi waje kuisapoti
timu yao uwanjani na nawahakikishia sitawaangusha,” alisema.
Kwa upande wake, Jaffar, alisema kuwa
wataendelea na zoezi hilo la usajili kwa kusajili wachezaji wengine kwa mujibu
wa mapendekezo ya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba.
“Kocha ameridhishwa na uwezo wa Wazir
(Junior), uongozi ukapambana kuhakikisha unapata saini ya mchezaji huyo na
hatimaye tumefanikiwa, ndio kwanza usajili tunauanza, lakini bado hizi ni kama
mvua sa lashalasha na masika yanakuja,” alisema.
No comments:
Post a Comment