Mkurugenzi wa Mawasiliano na
Teknolojia (TEHAMA) wa DAWASCO, Kiula Kingu akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es salaam wakati akitangaza uwepo wa mfumo mpya wa mawasiliano ambao
unalenga kumrahisishia mteja kupata na kutoa taarifa zinazohusu huduma hiyo kwa
haraka zaidi. Kushoto ni Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Everlasting Lyaro.
KATIKA kuhakikisha inarahisisha upatikanaji wa
huduma ya majisafi na kwenda na mfumo wa kisasa wa mawasiliano ya kiteknolojia,
Shirika la MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) limezindua mfumo mpya
wa mawasiliano ambao unalenga kumrahisishia mteja kupata na kutoa taarifa
zinazohusu huduma hiyo kwa haraka zaidi.
Huduma hiyo mpya sasa itapatikana kwa wakazi wote
wa jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani. Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Teknolojia (TEHAMA) wa
DAWASCO, Kiula Kingu amesema lengo kuu la mfumo huu ni kumweka mteja karibu
kihuduma na kila mwananchi ana uwezo wa kutumia mfumo huo katika simu yake
kupitia mitandao yote ya simu za mikononi nchini.
Kingu ameongeza kuwa ili mteja kunufaika na mfumo
huu anatakiwa kuhakikisha ana simu ya mkononi ya “Smartphone” ambayo
itamwezesha kupakua mfumo huo mpya wa DAWASCO, kisha kujisajili kwa kuingiza
akaunti namba yake ya DAWASCO ambapo baada ya kufuata hatua zote za kujisajili
mteja atatumiwa neno la siri ambalo litamwezesha kuingia na kupata taarifa
husika. “Sisi Dawasco tumeona haja ya kujiboresha na kwenda sawa na teknolojia
kwa kumletea mteja wetu mfumo rahisi ambao utamwezesha kupata taarifa zetu
kupitia simu yake ya mkononi muda wowote,”alisema Kingu.
Naye, Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Everlasting
Lyaro, amewataka wananchi wa Dar es Salaam na Pwani kupakua mfumo huu kwani ni
rahisi kuutumia na hauna gharama zozote. Anasema ni mfumo ambao utamrahisishia
mteja kupata taarifa muhimu zinazohusu huduma ya maji zikiwamo ankara ya mwezi,
taarifa za lini mteja alifungiwa huduma ya maji, muda ambao alifanya malipo,
lini mita yake ya maji ilisomwa na taarifa nyingine nyingi.
“Nawasihi wateja wetu na wananchi wote kupakua
mfumo huu mpya katika simu zenu za mkononi ili kuweza kufurahia huduma zetu,
hakuna gharama zozote ambazo utatozwa. Kupitia mfumo huu utaweza kupata taarifa
zote muhimu za huduma ya majisafi zikiwemo taarifa za mivujo ya maji na ankara
za maji za kila mwezi,”amefafanua Lyaro.
Anasema kwa sasa wateja hawana haja ya kutumia muda
mrefu katika ufuatiliaji wa kuunganishwa huduma ya maji, bali kilichorahisishwa
ni mteja kuweka taarifa zake sahihi kwenye mfumo huo na DAWASCO itatumia
taarifa hizo kumtafuta mteja na kukamilisha taratibu nyingine hadi kuhakikisha
mteja anapata huduma ya maji.
Katika kutimiza agizo la Waziri wa Maji na
Imwagiliaji, Mhandisi Greyson Lwengwe la kuhakikisha wakazi wa Dar es salaama,
Miji ya Kibaha na Bagamoyo wanapata huduma ya maji safi, DAWASCO imekua
ikijitahidi kuwafikia wananchi kwa njia na mbinu tofauti, kampeni tofauti kama
'mama tua ndoo ya maji kichwani' huku maunganisho ya maji kwa mkopo yakisaidia
upatikanaji na uboreshaji wa huduma ya maji kwa maeneo mengi ya jiji la Dar es
Salaam.
Mpaka sasa takribani watumiaji 25,000 wa mitandao
ya simu jijini Dar es Salaam wameshapakua mfumo huu na lengo la DAWASCO ni
kuwafikia wakazi wengi zaidi kwa kipindi kifupi.
No comments:
Post a Comment