Na Greyson Mwase, Pwani
Wilaya za Mkuranga, Kibiti na wilaya ya Rufiji katika kata ya Ikwiriri zimeanza kupata nishati ya uhakika ya umeme mara baada ya kuunganishwa katika Gridi ya Taifa na kukamilika kwa kituo cha kupozea umeme cha Mbagala kilichopo jijini Dar es Salaam.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati akizungumza na wananchi wa Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani katika ziara yake ya siku moja jana (tarehe 22 Machi, 2018) ya kukagua miundombinu ya umeme iliyounganishwa na Gridi ya Taifa kutokea katika kituo cha kupoza umeme cha Mbagala hadi Ikwiriri na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Dkt. Kalemani alisema lengo la kuunganisha wilaya hizo na Gridi ya taifa ni kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme wa uhakika na kuondokana na umeme unaotokana na mitambo ya mafuta ya Somangafungu ambayo imekuwa ikiharibika mara kwa mara.
Alisema awali kabla ya wilaya hizo kuunganishwa na Gridi ya Taifa, kulikuwepo na changamoto ya kukatika kwa umeme katika wilaya hizo kutokana na mitambo kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali iliamua kuunganisha wilaya hizo kwenye Gridi ya Taifa ili kuwepo na umeme wa uhakika ambao mbali na matumizi ya majumbani unategemewa na viwanda vilivyopo katika mkoa wa Pwani.
Katika hatua nyingine akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinyanya kilichopo katika wilaya ya Kibiti mkoani Pwani ambapo aliwasha rasmi umeme, Waziri Kalemani aliwataka wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini kupitia REA kuhakikisha vijiji vyote na vitongoji vyake vinapata umeme wa uhakika.
Aliwataka wakandarasi hao kuhakikisha sehemu za huduma muhimu za jamii kama vile vituo vya afya, shule, kanisa na misikiti zinapata umeme wa uhakika.
Waziri Kalemani pia aliwataka wananchi kuanza kutandaza mifumo ya umeme (wiring) majumbani pamoja na kulipia shilingi 27,000 kwa ajili ya kuunganishiwa na huduma ya umeme.
Alielekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha umeme haukatiki na kufungua ofisi karibu na wananchi ili kuepuka adha ya wananchi kwenda mbali kufuata huduma ya kuunganishiwa umeme.
“ TANESCO ni lazima mhakikishe mnawafuata wananchi na kukusanya fedha kwa ajili ya kuunganishiwa na huduma ya umeme, hata kama ni chini ya mwembe badala ya wananchi kutumia gharama kubwa kwenda mjini kuwafuata,” alisema Dkt. Kalemani
Wakati huohuo wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho waliishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma ya umeme na kuongeza kuwa uchumi wa wilaya ya Kibiti utaanza kukua kutokana na ajira kuongezeka.
Hamisi Mkwera akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake alisema uwepo wa umeme wa uhakika kwenye wilaya yao utachochea ukuaji wa viwanda na kuongezeka kwa fursa za ajira kwa wakazi waishio karibu na viwanda husika.
Mhandisi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Mhandisi Alex Adam (wa pili kushoto) akielezea shughuli zinazofanywa na kituo cha kupoza umeme cha Mbagala kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) katika ziara hiyo.
Mafundi wa kampuni ya Sengerema Engineering wakikamilisha ujenzi wa miundombinu ya umeme kwa ajili ya kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa katika kijiji cha Kinyanya kilichopo wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akibonyeza kitufe kuashiria uwashaji wa umeme katika kijiji cha Kinyanya kilichopo wilayani Kibiti mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment