Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori, akifungua pazia kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa mradi wa kuchakata majitaka unaojengwa katika Kata ya Mburahati, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, leo jijini hapa.
Katibu Tawala msaidizi huduma za maji Mkoa wa dar Mhandisi Elizabeth Kingu, akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo.
Mhandisi wa mradi wa uchakataji maji taka Mburahati, MOdekai Sanga, akifafanua jambo juu ya mradi huo kwa mgeni rasmi.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori, (kushoto) akisalimiana na Diwani Kata ya Mburahati, Yusuph Yenga, wakati wa uzinduzi rasmi wa ujenzi wa mradi wa kuchakata majitaka unaojengwa katika Kata ya Mburahati.
Afisa Uhusiano wa Shirika la Majisafi na Majitaka (DAWASA na Dawasco), Neli Msuye, (katikati) akiteta jambo na Mratibu wa Mradi, Laura Bright Davies (kushoto) wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa ujenzi wa mradi wa kuchakata majitaka unaojengwa katika Kata ya Mburahati.
Mratibu wa Mradi, Laura Bright Davies, akiwasalimia wananchi wa kata ya Mburahati katika hafla hiyo
SERIKALI Mkoani Dar es Salaam, imesema inamatumaini makubwa ya kuwapatia wakazi wake huduma ya maji kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2010 na asilimia 100 ifikapo mwaka 2025.
Pia, amesema kwa kushirikiana na Mamlaka zake za Majisafi na Majitaka (DAWASA na Dawasco) imejizatiti kikamilifu kukabiliana na changamoto ya uondoaji wa majitaka ambapo kwa sasa ni asilimia 10 tu ya wananchi mkoani humo wanapata huduma hiyo.
Akizindua ujenzi wa mradi wa kuchakata majitaka unaojengwa katika Kata ya Mburahati, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori, alisema sera ya serikali ni kuwafikishia huduma ya maji wananchi wake wote mkoani humo.
Makori ambaye pia alikuwa akihutubia katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji, mkoani humo, alisema, matumaini hayo yanatokana na miradi mikubwa iliyokamilika na mipango inayoendelea kutekelezwa na serikali kupitia DAWASA na DAWASCO na Ofidi ya Mkuu wa Mkoa.
“Kukamilika kwa mradi mkubwa wa Ruvu Chini ambao umeongeza upatikanaji wa maji kutoka lita milioni 182 kwa siku na kufikia lita milioni 270.
Kukamilika kwa mradi huu kutaongeza upatikanaji wa maji katika maeneo ya Bagamoyo,Tegeta, Mbweni, Kinondoni, Chuo Kikuu, Kunduchi, Kawe, Mikocheni na maeneo ya katikati ya jiji,”alisema Makori.
Pia, kukamilika kwa mradi mkubwa wa Ruvu Juu ambao alisema umeongeza upatikanaji wa maji kutoka lita milioni 82 kwa siku na kufikia lita milionui 196 kwa siku.
“Kumeongeza upatikanaji wa maji katika maeneo ya Kibaha, Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo na Tabata,”alifafanua.
Makori alisema kukamilika kwa visima 20 vya Kimbiji na Mpera vitaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa lita milioni 250 kwa siku maeneo yatakayohudumiwa na Wilaya ya Kigamboni, Temeke na baadhi ya maeneo ya wilaya ya Ilala.
“Kukamilika kwa miradi ya visima10 vya mpango wa maendeo ya sekta ya maji ambapo visima tisa vilivyojengwa na manispaa vinahudumia watu zaidi ya 300,000,”alisema.
Alisema hadi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la wateja waliounganishiwa huduma ya maji kutoka 123,00 mpaka 268,000.
Kuhusu suala la mfumo wa majitaka, Makori, alisema, kukamilika kwa ujenzi wa miradi midogo midogo ya kusafisha majitaka katika kata ya Toangoma na Mburahati itasaidia kwa kiasi kikubwa katika uondoaji wa majitaka katika makazi ya watu.
“Kwa sasa ni asilimia 10 tu ya wakazi ndiyo wanapata huduma ya kuondolewa majitaka lakini serikali kwa kuishirkiana na DAWASA na Dawasco, pamoja na wadau ipo katika hatua za utekelezaji miradi mikubwa,”alisema Makori.
Alitaja mradi mwingine wa mfumo wa uondoaji majitaka kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambao utajengwa katika eneo la Jangwani utakaokuwa na uwezo wa kusafisha zaidi ya lita za ujazo 200,000 kwa siku.
“Mradi wa Kurasini utakuwa unasafisha lita 11,000 kwa siku, Mbezi Beach utasafisha lita za ujazo 16,000,”alisema.
Aliongeza; ‘Mradi huu utahusu upanuzi wa mfumo wa majitaka maeneo ya katikati ya jiji, ujenzi wa mfumo mpya Ilala , Ubungo na Kinondoni,”
Alisema mradi wa maji na usafi wa mazingira unaofadhiliwa kupitia program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) utahusishwa na ujenzi wa mifumo 50 ya kukusanya na kusafisha majitaka na ujenzi wa vyoo vya kisasa na utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano.
Mhandisi wa mradi wa uchakataji wa maji taka Mburahati, MOdekai Sanga alisema utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 40,000 na utagharimu sh.milioni 95. za kitanzania, pia amewataka wanachi kutumia mradi huo vizuri kwamanufaa ya watanzania
No comments:
Post a Comment