Ujumbe wa viongozi wa wafanyabiashara kutoka nchini Ufaransa utatembelea Tanzania kwa muda wa siku tatu kuanzia Aprili 16 hadi 18, 2018, kwa ajili ya kuhudhuria Jukwaa la Kimataifa la Biashara pamoja na kuzungumza na serikali na viongozi wa biashara kuhusu uwekezaji.
Jukwaa hilo limeandaliwa na Chama cha Waajiri nchini Ufaransa-MEDEF kinachowakilisha asilimia 75 ya sekta binafsi nchini humo, chenye kampuni wanachama takribani 750,000, kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi nchini-TPSF, Ubalozi wa Tanzania Paris na Ubalozi wa Ufaransa Dar es Salaam.
Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier akizungumza kuhusu ujio wa viongozi wa wafanyabiashara kutoka nchini Ufaransa.
Ujumbe huo wa wafanyabiashara kutoka zaidi ya kampuni 30, unaoongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Biashara kati ya Ufaransa na Afrika Mashariki la MEDEF International, Momar Nguer utakutana na viongozi wa ngazi za juu wa serikali na wa TPSF na kuzungumza kuhusu kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili, na kufanya uwekezaji.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na wanahabari balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier amesema Kampuni za Ufaransa zinaridhishwa na uimara wa uchumi wa Tanzania pamoja na uwepo wa fursa nzuri za uwekezaji, na kwamba zimedhamiria kuanzisha ushirikiano mwema wa kibiashara baina ya kampuni za nchi zote mbili.
“Ili kufikia malengo hayo, kampuni za Ufaransa zinaahidi kuleta teknolojia ya hali ya juu, kushiriki kikamilifu kwenye miradi ya kijamii pamoja na kuleta ufumbuzi wa kudumu katika kuleta maendeleo,” amesema Clavier.
Jukwaa la Kimataifa la Biashara linalojulikana kwa jina la TPSF-MEDEF International Business Forum, litafanyika Jumatano ya Aprili 18 mwaka huuu katika Hoteli ya Serena iliyoko Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment