Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeuvaa upande wa mashtaka kutokana na kushindwa kutekeleza amri yake ya kumpeleka mmiliki wa IPTL, Harbinder Sethi kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kufuatia kutotekelezwa kwa amri hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi, amevitaka vyombo husika kuheshimu amri zinazotolewa na mahakama ikiwemo kuziekeleza.
Hakimu Shaidi amesema haipendezi Mahakama kila wakati kutoa amri ambzo hazitekelezwi, na kuamuru tena Mshtakiwa Sethi kupelekwa hospitali kabla hajatoa amri nyingine kwa mujibu wa sheria.
Awali, Wakili wa serikali, Nassoro Katuga amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, pia wameshindwa kumpeleka Sethi hospital kwa sababu maalumu ikiwemo Sethi kuhamishwa gereza kutoka Segerea kwenda Ukonga, pamoja na mshtakiwa huyo kuomba daktari wake kutoka Afrika Kusini awepo wakati akipatiwa matibabu.
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na Wakili wa utetezi, Hajra Mungula akidai hazina msingi kwa sababu Sethi hakuwahi kuzungumzia suala la daktari.Pia Mungula amedai kuwa katika gereza la Ukonga Sethi haruhusiwi kuonana na mtu yoyote hata mke wake wa ndoa.
Baada ya kutolewa hoja hizo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 25, 2018.
No comments:
Post a Comment